SIMBA WATUA MTWARA; KAGERE, OKWI NDANI

NA WINFRIDA MTOI


 

KIKOSI cha Simba kimewasili mjini Mtwara jana tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC ya huko, unaotarajiwa kupigwa kesho kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Simba waliondoka jana asubuhi kwa kutumia usafiri wa ndege, huku kikosi chao kikiwa na wachezaji 20, wakiwamo straika wao hatari, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Wachezaji nane wa timu hiyo wameachwa Dar es Salaam kuendelea na mazoezi chini ya Kocha Msaidizi, Masoud Djuma.

Mbali ya Okwi na Kagere, nyota wengine wa kutumainiwa Simba waliopo Mtwara na kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, ni Adam Salamba, Jonas Mkude, Marcel Kaheza, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein, Aishi Manula na Mohammed Ibrahim.

Wachezaji waliobaki ni Mohamed Rashid, Ally Salim, Mzamiru Yassin, Yusuph Mlipili, Abdul Khamis, Jjuuko Murushid, Hassan Dilunga, Asante Kwasi na wengineo.

Akizungumza na BINGWA juzi, Mbelgiji Aussems, alisema ameamua kukigawa kikosi hicho kutokana na kukabiliwa na michezo mitatu ya ugenini.

“Mtwara nitakuwa na wachezaji 20 pekee, wengine watabaki, mchezo si na Ndanda tu, ninafahamu tunakabiliwa na michezo mingine tena ya ugenini, hivyo siwezi kuwabeba wote,”  alisema.

Akizungumzia mchezo huo wa kesho, Aussems alisema anachohitaji ni pointi tatu, japo anafahamu anakwenda kukabiliana na timu ngumu ambayo hajaijua vizuri, ikiwamo mazingira ya uwanja watakaochezea.

“Mara nyingi viwanja vya ugenini vinakuwa vigumu, ndiyo maana tunawahi kwenda ili tukafanye mazoezi kwa siku mbili, ninazoamini zitatusaidia,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*