googleAds

Simba washtukia mchezo mchafu DRC

ZAITUNI KIBWANA NA HUSSEIN OMAR

HOMA ya pambano la robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na TP Mazembe, imezidi kupamba moto baada ya waamuzi wa mchezo wa marudiano kubadilishwa ghafla na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Simba wakiwa ugenini Lubumbashi, watarudiana na TP Mazembe Jumamosi kwenye Uwanja wa Stade TP Mazembe.

Ikumbukwe Simba ililazimishwa suluhu na TP Mazembe katika mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kuelekea mchezo huo wa marudiano, CAF imemteua Janny Sikazwe kutoka Zambia kuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Berhe Tesfagiorgis (Eritrea), Romeo Kasengele (Zambia) na Audrick Nkole mwamuzi wa mezani.

Wakati waamuzi hao wakipewa jukumu hilo, waliopangwa kuchezesha mchezo huo awali, Tessema Weyesa, kutoka Ethiopia na wasaidizi wake, Samuel Atango (Ethiopia), Gilbert Kipkoech (Kenya) na mwamuzi wa mezani, Peter Waweru (Kenya), wameenguliwa.

Kutokana na mabadiliko hayo, uongozi wa Simba kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Crescentius Magori, umetuma barua CAF ili kuomba kubatilisha uamuzi wa kubadilisha waamuzi wa mchezo huo wa marudiano.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Magori, Simba wameomba waamuzi waliopangwa awali wachezeshe mchezo huo kwani waamuzi wapya ni majirani na DR Congo, wakitokea Zambia.

Uongozi wa Simba umehofia marefa hao wapya kutoka Zambia kupangwa makusudi ili kuihujumu timu yao ukizingatia Zambia hadi Lubumbashi ni jirani mno kiasi kwa viongozi wa TP Mazembe kuwa na nafasi ya kuwafuata huko huko kwao ili kupanga mikakati ya kuwabania Wekundu wa Msimbazi hao.

Wakati barua hiyo ikitumwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili itumwe CAF, wanachama mbalimbali wa Simba, wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, wamekuja juu.

Zitto alitumia ukurasa wake wa Twitter akisema kuwa inawezekana kuna hujuma kwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa CAF, Constant Omari Selemani, anatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Waamuzi wamebadilishwa, wameondolewa waamuzi kutoka Ethiopia na Kenya na kuwekwa waamuzi kutoka Zambia. Natarajia viongozi wa Simba wanafuatilia suala hili maana inaweza kuwa ni hujuma hasa kwa kuwa Makamu wa Rais CAF anatoka Lubumbashi,” aliandika Zitto.

Licha ya mwamuzi huyo kulalamikiwa, Janny Sikazwe, amewahi kuchezesha fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.

Katika hatua nyingine, Wekundu wa Msimbazi hao wameandaa utaratibu wa mashabiki wao kwenda mjini Lubumbashi, DRC kuisapoti timu hiyo kwenye mchezo huo wa marudiano.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kila shabiki anayetaka kuifuata timu Lubumbashi atalazimika kulipa kiasi cha Sh 200,000 gharama ya usafiri wa barabara kwenda na kurudi pamoja na visa Dola za Kimarekani 50 (Sh 116,000).

Manara alisema pia kila shabiki atatakiwa kuhakikisha ameandaa fedha zake za malazi kiasi cha dola 20 hadi 25 kuendelea kwa siku moja kwenye hoteli, hiyo ni mbali ya gharama zake za chakula na nyingine muhimu.

“Mwisho wa kupokea uthibitisho wa safari hii ni leo saa 10:00 jioni,” alisema Manara.

Simba SC watalazimika kwenda kushinda mjini Lubumbashi au kupata sare ya mabao ili kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*