SIMBA WAINGILIA DILI LA MBENIN WA YANGA

ZAINAB IDDY NA SALMA MPELI


MPANGO wa Yanga kumsajili mshambuliaji wa Benin anayekipiga katika klabu ya Buffles du Borgou FC, Marcellin Degnon Koukpo unaonekana kuingiliwa na mahasimu wao Simba, ambao nao wameanza kuwasiliana na mchezaji huyo na kumweleza ukweli hali ya kiuchumi ya timu hiyo ya Jangwani kwa sasa.

Chanzo cha Habari ndani cha klabu hiyo inayoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kimesema wamewashtukia njama za mahasimu wao Simba, baada ya mchezaji huyo kuhoji masuala ya malipo akisema ameambiwa kwamba timu hiyo hailipi mishahara.

“Simba wameanza kutufanyia mtima nyongo kwa mchezaji wetu, mchezaji huyo ameanza kuhoji mambo kibao akisema ameambiwa kwamba Yanga hatulipi mishahara na fedha za usajili, hali hiyo imetutia shaka hata kushindwa namna ya kumleta Koukpo nchini,” kilisema chanzo hicho kikizungumza na BINGWA jana.

Simba wameonekana kuwa jeuri kutokana na kuwezeshwa na mfadhili wao mfanyabiashara Mohamed Dewij ‘MO’ na kuingilia usajili wowote pale, pindi wanapomtaka mchezaji anayewaniwa na klabu yoyote nchini na sasa wamevamia kwa Koukpo, kama ilivyokuwa kwa Adam Salamba kutoka Lipuli FC, Mohamed Rashid (Tanzania Prisons) na Marcel Kaheza aliyekuwa akifukuziwa na Coastal Union kimya kimya na kuwasajili wote.

Hivyo jeuri hiyo ya Simba, imewafanya Yanga kuficha mchakato wa kumleta nchini Koukpo, ambaye alitarajiwa kutua wiki hii ili kuja kumalizana na klabu hiyo ya Jangwani, lakini mpango huo wa kumleta nchini umebadilishwa.

“Koupko alitarajiwa kutua nchini Jumatatu au jana usiku lakini hatakuja kwa siku hizi mbili, hivyo uongozi umeamua kujipanga na kumleta kimya kimya mchezaji huyo ili wasije wakapokonywa tonge mdomoni,” kilisema chanzo hicho.

Lakini pamoja na Yanga kufichaficha ujio wa Koupko kila mara, BINGWA limepata taarifa za kuaminika kwamba mchezaji huyo atatua nchini Jumapili hii, ili kukamilisha usajili wake na klabu hiyo ya Jangwani.

Pia chanzo hicho kilikanusha taarifa zinazomhusisha Koupko na klabu ya Singida United, baada ya kuzagaa taarifa kuwa nao wameingilia dili la mchezaji huyo na ndio wanaowachongea Yanga, kikisema kwamba Simba ndio wanaohusika na mpango wa kuwachafua Wanajangwani.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwassa, ameweka wazi hilo akizungumza na gazeti dada la na BINGWA, DIMBA la Jumatano kusema wameamua kufanya usajili wao kimya kimya kwa ajili ya kukwepa hujuma zinazofanywa na wapinzani wao.

“Kuna timu zikisikia tunahitaji mchezaji fulani basi zinaingilia kati na kumsajili, tumeamua kufanya mambo yetu kwa usiri na muda ukifika tutaweka wazi ni nani tumemsajili,” alisema Mkwassa.

Kwa upande wa Simba, hakuna kiongozi aliyepatikana kukanusha tuhuma hizo za kuingilia mchakato wa usajili wa mahasimu wao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*