googleAds

SIMBA WAANDAE UCHAGUZI HURU

NA MWAMVITA MTANDA

UCHAGUZI Mkuu wa Simba uliopangwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu, umesimamishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kubaini mapungufu lukuki katika mchakato wake.

Mwenyekiti wa Uchaguzi TFF, Mwanasheria Revocatus Kuuli, alichukua hatua hiyo, baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba, kutangaza majina ya watu waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya klabu hiyo.

Kwa bahati mbaya, Kamati ya Uchaguzi ya Simba, chini ya mwenyekiti wake, Boniphace Lyamwike, ilikwenda katika mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo, ikiwa haijapatiwa mwongozo wa kanuni za uchaguzi.

Pamoja na Simba kufanya mabadiliko katika Katiba yao, lakini walitakiwa kuunda kamati ndogo ndogo, ikiwamo ya uchaguzi, nidhamu na maadili kabla ya kwenda katika mchakato wa kinyang’anyiro hicho.

Lakini kama walishindwa hilo, basi  Simba walitakiwa kutumia kanuni za uchaguzi za TFF kwa kuwa ni wanachama wa shirikisho hilo.

Kitendo cha Simba kuamua kufanya uchaguzi bila kuwapo kwa kanuni za uchaguzi ni kinyume cha mwongozo wa Katiba ya mfano ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Mwongozo wa Fifa upo wazi na  mwanachama wa TFF na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), wanatakiwa kuufuata pasipokukiukwa.

Sijaelewa kwanini waliingia katika mchakato wa uchaguzi bila kuangalia mwongozo wa Katiba ya mfano inahitaji kitu gani kabla ya kwenda katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.

Kwa kuwa Simba ni mwanachama wa TFF, walitakiwa kuangalia kanuni za uchaguzi zinataja wagombea wawe na sifa gani, ada ya kuomba kuwania uongozi, pamoja na sifa nyingine ambazo zipo katika kanuni hizo.

Lakini kama Simba wangeona ni mlolongo mrefu kutumia kanuni za uchaguzi za TFF, basi wangeacha mchakato wao wa uchaguzi mpaka pale ambapo wangeunda kanuni za kwao.

Haikuwa na haja ya mchakato wa uchaguzi wa Simba, kuweka kigezo cha shahada katika nafasi za kuwania uongozi wa klabu hiyo, kwa sababu hawakuwa na kanuni zilizokuwa zikiwaongoza katika mchakato wa uchaguzi huo.

Kwa maana hiyo, Simba pamoja na kufanya mabadiliko ya katiba yao yaliyobarikiwa na Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu nchini, lakini walishindwa kufanya hilo moja la kuunda kamati ndogo ndogo za kutenda haki.

Binafsi siamini kama Simba walikuwa hawajui kama wanakiuka kanuni, bali walitengeneza mazingira ya kuwabana baadhi ya watu ambao wangeingia katika mchakato wa uchaguzi huo, pengine wangewasumbua ndani ya sanduku la kura.

Ili uchaguzi wa Simba uweze kuwa huru na haki ni jukumu la viongozi wa Simba kuhakikisha wanafanyia kazi mapungufu yaliyobainika katika mchakato wa awali wa uchaguzi wa klabu hiyo.

Uchaguzi huru ambao hautatawaliwa na mizengwe, utaweza kupata viongozi bora ambao wataiongoza klabu hiyo kwa mafanikio makubwa, kuliko walivyojaribu kubana demokrasia na kuacha manung’uniko ya chini kwa chini miongoni mwa wanachama.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*