Simba tupo nyuma yenu

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, wanatarajiwa kucheza na timu ya JS Saoura ya Algeria katika mchezo utakaochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kwa Kundi D linaloundwa na timu za Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), JS Saoura na Simba.

Mchezo wa leo ni muhimu kwa Simba kupata ushindi ambao utaongeza morali ya wachezaji kushinda ule utakaofuata.

Lakini ushindi kwa Simba utatoa mwelekeo wa timu hiyo kufanya vizuri katika kundi lao hilo.

BINGWA tunasema Simba wana uwezo wa kupata matokeo mazuri wakiwa nyumbani kwa kujipanga vizuri uwanjani na kuhakikisha pointi tatu zinapatikana.

 Tunaamini Simba wakianza kwa ushindi watakuwa wamejiweka katika mazingira bora ya kutinga hatua ya robo fainali.

Tunasema kwamba, uwezo walioonyesha wachezaji wa Simba katika hatua ya awali ya ligi hiyo, wanatuaminisha wataweza kuendelea kuwapa furaha mashabiki wao.

 Tunaamini kwamba, kama Simba waliweza kuvuka makundi kwa kushinda michezo tatu iliyochezwa nyumbani na ugenini, hawatashindwa kuendeleza moto wao katika mchezo wa leo dhidi ya wapinzani wao.

Mwaka jana, Simba walianzia nyumbani kwa kuwafunga mabao 4-1 Mbabane Swallows ya Swaziland, baadaye kuwatoa kwa jumla ya mabao 8-1.

Katika mchezo wa marudiano, Simba walifanikiwa kuwafunga mabao 4-0 Mbabane Swallows uliochezwa ugenini, kabla ya kufungwa mabao 2-1 Nkana ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza, kisha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

BINGWA tunaamini Simba wanaweza kuendeleza wimbi la ushindi leo iwapo wachezaji wa timu hiyo watacheza kufa au kupona uwanjani.

Lakini tunatoa tahadhari kwa wachezaji wa Simba kutowadharau JS Saoura kwa kuwa wanakuja nchini wakiwa wamejipanga kwa lengo la kupata ushindi.

BINGWA tukiwa wadau wa kwanza wa michezo hususan soka, tunasema tupo nyuma ya Simba kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wa leo dhidi ya wapinzani wao, JS Saoura.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*