SIMBA POWER

  • Viongozi, wazee, mashabiki waungana kuimaliza AS Vita
  • Sasa Msimbazi nguvu moja, wachezaji washindwe wenyewe

NA ZAITUNI KIBWANA

KATIKA kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya AS Vita ya DR Congo na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, viongozi wa Simba, matawi na wanachama wamekutana katika kikao maalumu kujadili ni vipi wanaweza kuwachapa wapinzani wao hao.

Simba inavaana na AS Vita katika mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi, Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa Kundi D, utakaopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikao hicho kilifanyika jana makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Msimbazi, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 3:30 jioni na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Swedy Mkwabi na wajumbe wake, Selemani Harubu, Dk. Zawadi Kadunda na Asha Baraka.

Wakizungumza na BINGWA kwa nyakati tofauti, Katibu wa tawi la Ubungo, Ubaya Mkumbo, alisema agenda kubwa kwenye mkutano huo ilikuwa ni mchezo wao dhidi ya AS Vita.

“Kweli tumekutana, lengo ni kuhakikisha tunaibuka na ushindi na kupenya hatua ya robo fainali na hili linawezekana.

“Kuna mengi yapo ila kifupi tunajua mashushushu wa AS Vita wapo mjini na wanapata msaada wa karibu kutoka Yanga, hizo taarifa tunazo ila tunawaambia kama tuliweza kuwafunga Nkana hatua ya mtoano basi hata wao watakufa Taifa,” alisema.

Naye Omary Maslay ambaye ni Mwenyekiti wa Tawi la Kinondoni, alisema kuifunga AS Vita si kazi rahisi ndio maana viongozi wanahitaji ushirikiano wa kila mtu ndani ya Simba, kuanzia wazee, vijana, wachezaji, makocha, wadau wengineo na hata mashabiki wa kawaida.

“AS Vita ni timu iliyo kamili kila idara, hivyo na sisi tunapaswa kuweka mipango sawa ndio maana tunahakikisha ndani na nje ya uwanja mipango inakuwa sawa.

“Kuna watu toka juzi wanalinda Uwanja wa Taifa, tunajua wapinzani wana njia nyingi sana za kutumaliza hivyo tumejipanga kila idara,” alisema.

Kwa upande wake, Mkwabi alisema nguvu ya pamoja, ushirikiano na umoja ndio silaha pekee itakayoweza kuwasaidia kutimiza malengo yao ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

“Lengo ni kupanga mikakati, mbinu na kujilinda na hujuma zozote zinazoweza kujitokeza kuelekea mchezo huo, tumekutana kwa kuwa wote lengo letu ni moja la kutinga hatua robo fainali,” alisema.

Katika msimamo wa Kundi D la michuano hiyo, Simba inaburuza mkia ikiwa na pointi sita, huku JS Saoura ya Algeria ikiongoza na pointi nane, Al Ahly ya Misri ipo nafasi ya pili na pointi zao saba, sawa na AS Vita iliyopo nafasi ya tatu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*