Simba mmemsikia Tambwe

NA ZAINAB IDDY

WAKATI Wanamsimbazi wakiwa meno nje baada ya ushindi mnono wa jumla ya mabao 8-1 walioupata katika mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya Mbabane Swallows, mshambuliji wa Yanga, Amissi Tambwe, amewaambia si wakati sahihi wa kutabasamu kwao.

Simba imepata ushindi huo mnono kwenye mechi zake mbili za Ligi ya Mabingwa, mchezo wa kwanza walicheza jijini Dar es Salaam na kushinda 4-1 kabla ya juzi kupata tena ushindi wa bao 4-0 Swaziland.

Matokeo hayo ya Simba yanawapa nafasi ya kusonga mbele na huenda wakakutana na timu kati ya Nkana Red Devils ya Zambia au UD Songo kutoka Msumbiji kati ya Desemba 15 au 16 kabla ya kurudiana Desemba 27 na 28 mwaka huu.

Tambwe ameliambia BINGWA kuwa ni mapema sana Simba kuanza kufurahi na kujihakikishia watafika hatua ya makundi kwa kuwa kila wanavyosonga mbele ndivyo ugumu wa mashindano hayo unaonekana.

“Ni mapema sana Simba kufurahia matokeao, kwani mashindano haya yana tabia ya kuwa magumu kila mnavyopiga hatua, hivyo ni bora wakafanya kama hakuna kilichotokea.

“Kwa sasa jambo la muhimu kwao ni kujipanga kwa mechi inayofuata huku wakijua hatua ya mbele ni ngumu zaidi, wasijiamini sana kwani mpira una matokeo ya ajabu sana,” alisema.

Tambwe aliongeza kuwa: “Binafsi nawapongeza wameonyesha mpira mzuri katika mechi zote mbili, nina hakika wakijiona si lolote si chochote kwa timu watakazokutana nazo mbele na kujipanga watafika mbali.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*