Simba, Js Saoura kesho hapatoshi makocha watunishiana misuli

LULU RINGO, DAR ES SALAAM

Kuelekea mchezo wa hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya Simba SC na Js Saoura ya nchini Algeria, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam makocha wa timu zote mbili wamejitamba kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Makocha hao wamezungumza na waandishi wa habari leo Jabuari 11, kila mmoja amejitamba kushinda mchezo huo.

Kocha wa magolikipa wa Simba SC, Mwarami Mohamed amesema licha ya nchi ya Algeria kuwa katika kiwango bora cha soka barani Afrika dhumuni kubwa ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili wafanye vizuri

“Tunawaheshimu Algeria tunajua wako kwenye kiwango kizuri cha soka Afrika, hata timu yao pia ni nzuri, lakini tumejipanga kushinda mchezo wa kesho katika uwanja wetu wa nyumabani” amesema Mwarami.

Kwa upande wa Kocha wa Js Saoura, Neghiz Nabil amesema kundi walilopangwa lina changamoto kubwa kutokana na ubora wa timu ya Simba na Al Ahly ya Misri lakini furaha yake kubwa ni kurejea Algeria akitoka Tanzania na alama tatu.

“Kundi tulilopangwa ni gumu, kuna timu ya Simba na Al Ahly ambazo zinafanya vizuri sana, kocha wa Simba ni kocha mzuri lakini kesho lazima tuondoke na ushindi,” amesena Neghiz.

Timu ya Simba na Js Saoura (Algeria) wamepangwa kundi D pamoja na timu ya Al Ahly (Misri) na AS Vita (Congo).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*