Simba jeuri nyie

*Watamba eti Ajib si wa kuweka kambi Moro

*Waahidi ‘surprise’ nyingine ya aina yake

NA WINFRIDA MTOI

KLABU ya Simba, imesema kuwa imewachukua muda kidogo kupata kambi ya timu yao, kwani walitaka kupata sehemu inayolingana na hadhi ya nyota wao, akiwamo Ibrahim Ajib aliyetokea Yanga.

Simba imetoa tambo hizo, ikiwa ni saa chache baada ya Yanga kutua mjini Morogoro kuweka kambi ya kuanza kuuwinda msimu ujao, wakikabiliwa na kibarua cha Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo kwa Wekundu wa Msimbazi.

Tayari Simba imetangaza kuweka kambi Afrika Kusini, wakitamba kupata hoteli ‘bab kubwa’, wakiamini itawawezesha wachezaji wao kujifua vilivyo, lakini pia kuyashika maelekezo ya makocha wao, wakiongozwa na mkuu wa benchi la ufundi, Patrick Aussems. 

Akizungumza na BINGWA jana, mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi kwa madai ya kuepuka kurushiwa mawe na watu wa Yanga, alisema kuwa kwa hadhi ya wachezaji waliowasajili msimu huu, si sahihi kuweka kambi hapa nchini.

“Kambi unaweka sehemu inayolingana na hadhi ya wachezaji wako, hatuwezi kwenda kuweka kambi sehemu kama Morogoro au Singida, tumetafuta sehemu yenye hadhi ya juu ili kuwaandaa ipasavyo wachezaji, wakirudi huku wamekuwa wameiva, wanaonyesha kile walichokipata mazoezini,” alisema.

Simba iliwahi kuweka kambi katika hoteli ya Petra iliyopo Johannesburg ambayo nayo ipo katika mpango wao, lakini kwa sasa wanamsubiri Aussems ili achague atakayoona inamfaa zaidi.

Juu ya kambi yao, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, aliliambia BINGWA akisema kama walivyosajili wachezaji wakubwa, hata kambi inatakiwa kuwa ya kiwango cha juu.

“Tumesajili wachezaji wa kiwango cha juu, itashangaza kama wachezaji kama hao, ukawapeleka katika kambi ya ajabu ajabu,” alitamba.

Aliongeza: “Kama tulivyosema, safari hii hatukurupuki katika kambi kama tulivyofanya kwenye usajili, tumechukua wachezaji wa kiwango cha juu watakaotufikisha mbali zaidi ya pale tulipofika msimu uliopita, lakini pia lazima wakaandaliwe katika kambi bora.”

Alisema baada ya kocha wao kuwasili, wachezaji wao wataanza mara moja safari ya kuelekea kambini kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa pamoja ‘Simba Day’.

Mbali ya Ajib, wachezaji wapya waliotua Simba ni nyota watatu kutoka Brazil, Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Vieira na Wilker Da Silva, lakini pia Msudan Sharaf Ali Abdalrahman.

Wengine ni Francis Kahata (Gor Mahia, Kenya), Deo Kanda (TP Mazembe, DR Congo), Beno Kakolanya (Yanga) na Kenedy Juma (Singida United).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*