Simba jeuri 100%

HUSSEIN OMAR

PAMOJA na kufungwa mabao 2-1 na Nkana katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wameonekana kutotishwa na kipigo hicho wakiamini wana uwezo wa kupindua matokeo jijini Dar es Salaam na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Baada ya kupoteza mjini Kitwe, Zambia, Simba watarudiana na Nkana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili hii, huku Wekundu wa Msimbazi hao wakitakiwa kupata ushindi wa zaidi ya bao 1-0.

Timu itakayopita katika raundi hiyo ya kwanza baina ya Simba na Nkana, itatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Na kutokana na jinsi walivyopania kufanya makubwa katika michuano hiyo, muda mfupi baada ya kurejea nchini kutoka Zambia juzi, kikosi cha Simba kiliingia moja kwa moja kambini kuwawinda wapinzani wao hao.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walirejea nchini juzi usiku kutoka Zambia na kwenda moja kwa moja kambini katika Hoteli ya Sea Scape iliyopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa Simba, Abbas Ally, alisema kuwa wameweka kambi katika Hoteli ya Sea Scape iliyopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam na jana jioni walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterans, uliopo Boko, jijini.

“Tumerudi jana (juzi), timu imekwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo wa marudiano, kila kitu kipo sawa, wachezaji wamejua wapi walikosea na kupoteza mchezo ule,” alisema Ally.

Alisema Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amebaini Nkana walisaidiwa zaidi na nguvu kutokana na wachezaji wao kuwa na miili iliyoshiba, hivyo ameshapata dawa ya kuwadhibiti.

“Unajua wale jamaa wana nguvu sana, lakini pia wana miili mikubwa na stamina ya hali ya juu, ndio maana mwalimu kaamua timu ikae kambini tangu tuliporudi,” alisisitiza Ally.

Kuelekea mchezo wa marudiano, Mbelgiji Aussems amesema kuwa amepanga kuwapa dozi kamili wachezaji wake ili kuwamudu wapinzani wao hao.

Aussems alisema amebaini kuwa kiungo wa Nkana, HarrisonChisala, ndiye alikuwa hatari zaidi katika safu ya kiungo na kuwapoteza viungo wake, hivyo amejipanga vilivyo kumzima.

“Ni lazima tufanye kazi ya ziada kuwadhibiti wapinzani wetu,lakini kwangu mimi Chisala alikuwa hatari zaidi na alicheza vizuri katika sehemu ya kati na kutupoteza,” alisema Aussems.

Aussems alishatamba kuifikisha mbali Simba katika michuano hiyo, akiamini kutokana na ubora wa kikosi chake, hakuna litakaloshindikana.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*