googleAds

SIMBA: HATUJAMTELEKEZA AVEVA

TIMA SIKILO NA JAPHARY LESSO (DSJ)

UONGOZI wa Simba umesema madai ya kwamba wamemtelekeza Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva aliyelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, hayana ukweli wowote.

Rais huyo wa Simba ambaye amekuwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi ya utakatishaji wa fedha, alipelekwa Hospitali ya Temeke, jijini na baadaye kuhamishiwa Muhimbili kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa figo.

Akizungumza na BINGWA kwa simu akiwa Arusha jana, Katibu Mkuu wa Simba, Dk. Anorld Kashembe, alisema kuna viongozi wa juu wa klabu yao walikwenda kumjulia hali na kwamba hawawezi kumtupa mwenzao huyo hasa katika kipindi hiki.

“Mimi nipo Arusha natarajia kurudi kesho(leo), lakini hizo taarifa zinazodai kuwa Rais (Aveva) ametelekezwa hazina ukweli wowote, kwani kuna viongozi ambao walikwenda kumjulia hali hospitalini na hali yake inaendelea vizuri,” alisema Kashembe.

Alisema miongoni mwa viongozi waliokwenda kumjulia hali Aveva ni Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ pamoja na Kaimu Makamu, Iddi Kajuna, ambao walithibitisha kuwa hali yake inaendelea kuimarika.

Aveva Jumapili ya wiki iliyopita alikimbizwa Hospitali ya Temeke baada ya hali yake kubadilika akiwa mahabusu katika Gereza la Keko, jijini kabla ya kuhamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*