SIMBA HAKUNA KULALA

NA MWAMVITA MTANDA


WEKUNDU wa Msimbazi Simba, wametua alfajiri ya leo wakitokea nchini Uturuki ambako waliweka kambi takribani wiki mbili kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania ambayo inatarajia kutimua vumbi Agosti 22, mwaka huu.

Licha ya kwamba wanatoka safari ya mbali, lakini bado kikosi hicho hakipo tayari kulala na badala yake watafanya mazoezi leo chini ya kocha wao, Mbelgiji, Patrick Aussems, katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Kikosi hicho kilifunga rasmi kambi yake juzi huko nchini Uturuki na baada ya kutua leo, wataendelea na mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya kibarua kizito ambacho kipo mbele yao cha mechi kali dhidi yao na Asante Kotoko ya Ghana.

Akizungumza na BINGWA jana, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma, alisema hawana muda tena wa kupoteza, inawalazimu kutua na kuanza mazoezi haraka kutokana na mechi hiyo ngumu iliyopo mbele yao.

“Hatuna muda kabisa wa kupoteza, japokuwa tumetoka safari ya mbali lakini kwa kipindi hiki sisi kwetu hata sekunde ni mali, tunatakiwa kuzingatia sana, hivi kesho (jana) tukitua tu jioni lazima tuingie mazoezini,” alisema Djuma.

Pia kocha huyo alisema, kikosi cha Simba cha msimu huu si cha kawaida, namba zimekamilika hivyo wachezaji wanahitaji mazoezi ya kutosha ili kukabiliana na mechi mbalimbali.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*