‘SIMBA CHAGUENI WATAKAOENDANA NA MFUMO MPYA’

NA WINFRIDA MTOI


 

KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa klabu ya Simba, uongozi wa klabu hiyo umewataka wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi watakaoendana  na muundo mpya wa timu na si wakushindana na Yanga.

Simba wanatarajia kufanya Mkutano Mkuu na uchaguzi, Jumapili katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Siku hiyo kutakuwa na mikutano miwili, utaanza Mkutano Mkuu wa kila mwaka saa 2:30 asubuhi hadi 6:00 na mkutano wa uchaguzi utaanza saa 7:30 mchana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema  matarajio yao ni kuona wanachama wa Simba wanakwenda kuchagua kiongozi atakayeendana na mahitaji ya klabu hiyo kwa sasa.

Alisema klabu hiyo ipo katika muundo mwingine na kiongozi anayeingia madarakani atambue kuwa anakwenda kujitolea kuhakikisha Simba inajiendesha kiuchumi na kupigania makombe makubwa.

“Tunaratajia kuona wanachama wanakwenda kuchagua viongozi ambao hawana mashaka katika kutekeleza mahitaji ya klabu ya Simba katika muundo mpya uliopo.

“Simba ya sasa haihitaji kushindana na Yanga wala kupigania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara bali makombe ya kimataifa yenye hadhi na uelewa wa kuipeleka Simba mbele,” alisema Manara.

Katika hatua nyingine, Manara amepongeza jinsi mchakato wa uchaguzi ulivyokuwa na utulivu na kusema ni tofauti na chaguzi nyingine zilizopita na hadi kufikia sasa hakuna kashfa yoyote ya rushwa.

Alisema hali hiyo inatokana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kutupia jicho katika uchaguzi huo pamoja na wagombea  waliopitishwa kuwa makini na kufanya kampeni zao kistaarabu.

“Tunawaomba wanachama wasiolipa ada zao za uanachama wafanye hivyo, ili wapate fursa ya kushiriki mkutano na uchaguzi, pia kuelekea uchaguzi huu kuna wanachama wapya zaidi ya 200, kadi zao ziko tayari na wataruhusiwa kushiriki mkutano huo,” alisema Manara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*