Simba, Azam zitupe burudani

NA MWANDISHI WETU

SIMBA na Azam zinatarajia kushuka uwanjani leo kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii wa kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/20.

Mchezo huo  ataanza saa moja usiku kwenye Uwanja wa Taifa, jijini  Dar e Salaam, ambapo  Simba ni mabingwa wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Azam mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Tunaamini mchezo wa leo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na jinsi timu hizo mbili zilivyofanya maandalizi kuhakikisha zinapata ushindi.

Pamoja na mchezo wa Ngao ya Jamii utakuwa wa utangulizi wa Ligi Kuu Bara lakini tunaona utakuwa na faida mara  mbili kwa timu zote mbili zinazojiandaa pia na michezo ya marudiano ya kimataifa.

Katika michuano hiyo ya kimataifa, Simba watacheza na UD Songo ya Msumbiji ukiwa ni mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kati ya Agosti 24,mwaka huu,  kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya Wekundu wa Msimbazi kupata suluhu ugenini.

Kwa upande wa Azam watautumia mchezo wa Ngao ya Jamii kurekebisha makosa yao, baada ya kufungwa na Fasil Kanema ya Ethiopia bao 1-0 katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa  Jumapili iliyopita ugenini na kutarajiwa kurudiana Agosti 23,mwaka huu, Dar es Salaam.

Lakini mchezo wa Ngao ya Jamii utatoa taswira kwa timu zote mbili kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaoanza Agosti 23.

Tunaamini kuwa mchezo leo utakuwa ni burudani tosha kwa mashabiki wa Simba na Azama na Watanzania wengine kwa ujumla.

BINGWA tunasema kuwa haturajii kuona wachezaji wakikamiana uwanjani kupita kiasi na kusababisha kupoteza ladha ya mchezo wenyewe.

Kwa upande wetu tunaamini kuwa kila timu itaonyesha soka la kiufundi zaidi kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wao na si vinginevyo.

Tunazitakia kila la heri Simba na Azam  katika mchezo wa kiungwana


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*