googleAds

SIMBA 0-0 TP MAZEMBE…Pengine Simba wanahitaji kutuonyesha maajabu ya Manchester United, Ajax

NA AYOUB HINJO

REKODI ya Simba kushinda michezo yote kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ilishindwa kuendelea baada ya kulazimishwa sare ya kutofungana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa kiasi kikubwa mashabiki wa Simba waliingia uwanjani wakiwa na uhakika wa kushinda mchezo huo, kwani tayari timu yao ilifanikiwa dhidi ya Mbabane Swallows (eSwatini), Nkana FC (Zambia), JS Saoura (Algeria), Al Ahly (Misri) na AS Vita (DR Congo).

Ni rahisi kusema Simba waliufanya Uwanja wa Taifa kuwa machinjio kwa wapinzani wao, ni rahisi kwa wageni kuingia na presha sehemu yenye rekodi nzuri. Mara nyingi huwa hivyo.

Pamoja na mchezo huo kumalizika pasipo kufungana, gazeti la BINGWA linakuletea uchambuzi wa kina juu ya mechi hiyo kabla ya marudiano yatakayochezwa jijini Lubumbashi, Aprili 13 mwaka huu.

KUUELEWA MCHEZO

Sare hiyo haina faida upande wowote, sababu kila timu inayo nafasi ya kufanya chochote ili wajipatie tiketi ya kutinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo bado mpya kwa timu zote mbili lakini inawezekana juzi kulikuwa na uelewa tofauti wa mechi hiyo kali kwenye Uwanja wa Taifa.

Pamoja na Simba kuhitaji ushindi ili kuweka mazingira mazuri katika mechi ya marudiano, bado walishindwa kutegua mitego ya TP Mazembe.

Kivipi? Ni wazi wakali hao kutoka DRC walicheza nyuma ya mpira kwa kiasi kikubwa na hilo kuwafanya Simba kushindwa kuvunja ngome yao ya ulinzi kwa urahisi.

Kwa kiasi kikubwa Simba walilazimishwa kucheza mpira pembeni ambako kulikuwa na Haruna Niyonzima na Clatous Chama kabla ya Mzambia huyo kutoka na nafasi yake kuchukuliwa na Emmanuel Okwi.

Eneo la kiungo lilikuwa gumu kwa Simba kupitisha mipira ya kupenyeza kwa washambuliaji wao, Meddie Kagere na John Bocco ambao kwa kiasi kikubwa walipigiwa mipira mirefu ya kukimbia ili kuvuka eneo la kati.

Kwa kifupi, hakukuwa na ubunifu zaidi ambao ungewafanya wapinzani wao kufanya makosa katika eneo lao mwisho na kutumiwa kama faida na Simba.

Sijui kwanini Mzamiru Yassin au Hassan Dilunga hawakupewa nafasi, ni wachezaji wawili tofauti ambao wanaweza kufanya kazi moja uwanjani.

Mzamiru ni mchezaji anayefanya mambo mawili uwanjani, ana uwezo wa kufanya ‘recovering’ kila mpira unapokuwepo na kuisukuma timu kwenda mbele, pia ana uwezo wa kufunga mabao nafasi zikipatikana.

Dilunga kama anavyojulikana kwa kurahisisha kazi kwa washambuliaji wake, ana uwezo wa kutengeneza nafasi za mabao kwa kupiga pasi za kupenyeza.

Pamoja na yote, bado faida ipo kwa timu zote mbili kuweza kufanya chochote kwenye mechi ya marudiano.

Ili kuwe na uhakika wa Simba kusonga mbele lazima watumie nafasi zinazotengenezwa vizuri, juzi walishindwa kufunga katika nafasi nne ambazo zilitengenezwa sambamba na ile penalti iliyokoswa na nahodha Bocco.

MCHEZO WA MARUDIANO

Kocha wa Simba, Patrick Aussems, si muoga kushambulia anapokuwa ugenini japo hakuna mchezo katika hatua ya makundi waliofanikiwa kushinda au hata kufunga bao.

Mechi pekee ambayo Simba walishinda ugenini ilikuwa dhidi ya Mbabane Swallows hatua ya awali; walishinda mabao 4-0.

Ni rahisi kutambua kuwa TP Mazembe watacheza mchezo tofauti kama ilivyokuwa kwenye Uwanja wa Taifa, watahitaji kutengeneza nafasi za uhakika ili kufunga mabao.

Itakuwa hivyo kwa Simba pia ambao wanahitaji ushindi au kulazimisha sare ya mabao ili wasonge mbele.

Yote hayo ili yawezekane inabidi wacheze mchezo wa kushambulia au hata kama wa kuzuia, lakini wawe na uhakika wa kufika langoni kwa TP Mazembe.

Katika uwanja wa TP Mazembe, hakuna wapinzani waliofanikiwa kufunga bao kwenye hatua ya makundi, je, Simba wataweza kuvunja mwiko huo?

Katika mchezo wa soka chochote kinawezekana, pengine mifano hai hivi karibuni ni maajabu yaliyoonyeshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na timu za Manchester United ya England na Ajax ya Uholanzi.

Manchester United waliwatoa PSG ya Ufaransa kwa kuwafunga mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Parc de Princes, baada ya vigogo hao wa England kukubali kichapo cha mabao 2-0 ndani ya Old Trafford.

Nao Ajax walishinda mabao 4-1 dhidi ya Real Madrid ya Hispania katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, licha ya kufungwa mabao 2-1 nchini Uholanzi na waliokuwa mabingwa wa Ulaya mara tatu mfululizo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*