SERIKALI YATENGA SH BIL 1.2 AFCON YA VIJANA

NA ELIZABETH HOMBO, DODOMA
SERIKALI imetenga Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 zilizopangwa kufanyika mwakani hapa nchini.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe,  alisema  bungeni jana, wakati akijibu swali la Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro (CCM),  aliyetaka kujua kama Serikali ina bajeti kwa ajli ya timu za Taifa zinazobeba bendera kuitangaza nchi kimataifa.
Akijibu swali hilo la Dk. Ndumbaro lililoulizwa kwa niaba yake na Venance Mwamoto (Kilolo-CCM), Dk. Mwakyembe alisema Serikali inatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya michezo nchini ambayo inaendana na ukubwa wa mashindano yanayoikabili.
“Kwa mfano, mwakani Tanzania ni mwenyeji wa mashindano ya soka ya Afcon kwa vijana chini ya umri wa miaka 17.
“Hivyo mbali na vyanzo vingine vya fedha, Bunge hili tukufu limeidhinisha Sh bilioni moja itumike kuboresha miundombinu ya Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru na Sh milioni 293.6 kwa maandalizi mengine,” alisema.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu, alihoji Serikali ina mpango gani wa kuboresha jukwaa la VIP katika Uwanja wa Taifa ambalo halina kibanda au kinga ya jua au mvua wakati hali ya hewa inabadilika?.
Akijibu hilo, Dk. Mwakyembe alisema, “Ni kweli kuna mapungufu katika uwanja wetu wa taifa na ndiyo maana tulipokuja kuomba tutengewe fedha za ukarabati wa uwanja wa taifa mlikubali.”
Aidha, alisema kiasi cha Sh bilioni moja kilichotengwa kitakwenda kufanya mabadiliko na katika siku za usoni watarajie kuona marekebisho hayo.
Awali kabla ya kujibu maswali hayo, Dk. Mwakyembe aliwapongeza Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/18, timu ya Simba kwa kutinga fainali ya michuano ya Sportpesa Super Cup nchini Kenya.
“Nawapongeza mabingwa wa Tanzania Bara kwa kutinga fainali ya Sportpesa, Simba wamethibitisha kuwa walipata ubingwa si kwa kubahatisha bali kwa soka la viwango na sasa wanaingia fainali kupambana na mabingwa wa Kenya Gor Mahia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*