Serengeti Boys yapoteza bahati mbaya

MAREGES NYAMAKA NA WINFRIDA MTOI

KWA bahati mbaya kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, kimepoteza mchezo wa kwanza wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kuchapwa mabao 5-4 na Nigeria.

Nigeria walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Olatomi Olaniya katika dakika ya 20 ya mchezo huo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kabla ya Serengeti Boys kusawazisha muda huo huo kupitia kwa Edmund John, akitumia pasi ya Kelvin John ‘Mbappe’.

Lakini baadaye Nigeria walifunga mabao mengine dakika ya 29 na                                36 kupitia Wisdom Ubani na Akinkunmi Amoo na timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa mabap 3-1.

Kipindi cha pili Serengeti Boys walirudi kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha mabao hayo na kuongeza kupitia nyota wake, Mbappe katika dakika ya 51, huku bao la tatu na la nne yakifungwa kwa mikwaju ya penalti na Morice Abraham dakika ya 56 na Edmund John dakika ya 59.

Baada ya Serengeti Boys kuwa mbele, walionekana kutawala mchezo huo na kupoteza nafasi kadhaa za mabao, lakini baadaye Nigeria walizinduka na kuanza kulishambulia lango la vijana hao wa Tanzania.

Katika dakika ya 71, Nigeria walitumia vizuri makosa ya mabeki na mlinda mlango wa Serengeti Boys kusawazisha kupitia Ubani na dakika nane baadaye Samson Tijan kufunga la ushindi.

Mchezo huo ulishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, aliyekuwa mgeni rasmi na kutoa agizo la mashabiki kuingia bure katika michuano hiyo ili kuongeza hamasa.

Serengeti Boys watashuka tena dimbani kesho kuvaana na Uganda katika mchezo wao wa pili ambao utachezwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*