googleAds

Serengeti Boys wapo tayari kuanza safari ya Brazil 

NA ISIJI DOMINIC

MAWAZO ya timu ya soka ya Tanzania kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 maarufu Serengeti Boys, yameelekezwa nchini Brazil ambapo michuano ya Kombe la Dunia itafanyika baadaye mwaka huu.

Lakini ili kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys watahitajika kupambana na kutinga hatua ya nusu fainali Kombe la Afrika kwa umri huo ambapo Tanzania tutakuwa wenyeji.

Michuano hiyo kanda ya Afrika ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), imepangwa kuanza Jumapili hii jijini Dar es Salaam na itachezwa kwenye viwanja viwili; Uwanja wa Taifa na Azam Complex.   

Serengeti Boys imekuwa kambini kwa muda mrefu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limehakikisha wanapata maandalizi ya kutosha ikiwemo kushiriki michuano mbalimbali. Katika kila michuano ambayo vijana wetu wameshiriki, wametoa matumaini Taifa Stars ijayo kuwa imara.

2018 CECAFA U-1

Aprili 19 hadi 29 mwaka jana katika miji ya Ngozi, Muyinga na Gitenga nchini Burundi, Serengeti Boys ilikuwa miongoni mwa timu nane zilizoshiriki Kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 inayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Tanzania ilikuwa kundi moja na Uganda, Sudan na Zanzibar ambao hata hivyo walitolewa baada ya kugundulika kuchezesha ‘vijeba’. Katika mechi mbili walizocheza hatua ya makundi, Tanzania waliambulia sare ya bao 1-1 na Uganda kabla ya kuitandika Sudan 6-0.

Mchezo wa nusu fainali ulikuwa mkali na wa kuvutia na Serengeti Boys waliwafunga Kenya 2-1 kabla ya kuizima Somalia 2-0 mchezo wa fainali na kutwaa ubingwa wa CECAFA chini ya umri wa miaka 17.

Kanda ya Kati-Mashariki

Tanzania ilikuwa mwenyeji wa michuano ya kufuzu Kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 kutoka ukanda wa CECAFA. Jumla ya mataifa tisa ambayo yaligawanywa katika makundi mawili yalishiriki michuano hiyo iliyofanyika kuanzia Agosti 11 hadi 26 mwaka jana.

Kundi A ambayo Serengeti Boys walikwemo walichuana na Rwanda, Burundi na Sudan ambapo vijana wa nyumbani walianza kampeni vizuri kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Burundi. Mchezo uliofuata ulikuwa dhidi ya Sudan na Serengeti Boys kushinda 5-0 kabla ya kuitandika Rwanda 4-0.

Katika mchezo wa nusu fainali, Serengeti Boys walipoteza 3-1 dhidi ya Uganda lakini waliambulia ushindi wa mabao 4-3 kwa penalti dhidi ya Rwanda kutafuta mshindi wa tatu baada ya timu zote kumaliza mechi kwa sare ya mabao 2-2.

UEFA Assist  

Michuano mingine iliyoipa mazoezi Serengeti Boys ilikuwa UEFA Assist iliyofanyika mwezi uliopita jijini Antalya, nchini Uturuki.

Timu zote ambazo zitachuana Kombe la Afrika kwa vijana zilishiriki pamoja na Australia kutoka Bara la Asia, huku wakiwakilisha kutoka Chama cha Soka Ulaya walikuwa Belarus, Montenegro na wenyeji Uturuki. Zilikuwa mechi muhimu za kujipima nguvu na moja ya hiyo mechi ilikuwa dhidi ya Australia ambapo Serengeti Boys walitoka nyuma na kushinda 3-2.

Michuano maalumu Rwanda

Hivi karibuni, Serengeti Boys walisafiri kwenda Rwanda kwa michuano maalumu iliyoshirikisha timu tatu; Tanzania, Rwanda na Cameroon. Serengeti Boys walianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Cameroon kabla ya kutoa sare ya mabao 3-3 na wenyeji Rwanda. Sare hiyo ilitosha kuipa Serengeti Boys taji hilo kwa sababu Rwanda walipoteza 3-1 katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Cameroon.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*