googleAds

Serengeti Boys kuweka kambi Korea Kusini

NA ZAITUNI KIBWANA

KIKOSI cha vijana chini ya miaka 17  ‘Serengeti Boys’, Novemba mwaka huu, kinatarajia kuweka kambi Korea Kusini ambako itacheza mechi mbalimbali kujiweka vizuri kwa ajili ya kupeperusha bendera ya taifa.

Hayo yamesemwa jana na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, ambaye amesema lengo la kambi hiyo ni kuwapa uzoefu wa michezo ya kimataifa.

Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza vijana hao walioshindwa kukata tiketi ya fainali za Afrika mwakani Madagascar, Malinzi alisema timu hiyo sasa inapandishwa na kuunda kikosi cha vijana chini ya miaka 20, ‘Ngorongoro Heroes’.

“Userengeti umefutwa na hawa vijana ndio watakaounda Ngorongoro Heroes, hivyo watakwenda Korea Kusini kupata uzoefu zaidi wa mechi za kimataifa,” alisema Malinzi.

Katika hatua nyingine, kocha mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime, aliyemwaga machozi hadharani, alisema kipigo walichokipata dakika za lala salama kamwe hawezi kukisahau maishani.

Naye mgeni rasmi kweye hafla hiyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, kazi, Ajira, Bunge, Vijana na Walemavu, Dk. Possy Abdallah, aliwataka vijana hao kuendeleza nidhamu waliokuwa nayo ili wafike mbali.

“Bila nidhamu tutakuwa tunajidanganya, utaona hata wenzetu wanasonga mbele kutokana na nidhamu ya wachezaji waliokuwa nayo,” alisema.

Serengeti Boys inatolewa kwa bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 3-3, kufuatia kushinda 3-2 katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*