googleAds

SERENGETI BOYS ISAIDIWE KWA NGUVU ZOTE

TIMU ya soka ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, imefanikiwa kupata nafasi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Gabon, Aprili mwaka huu.

Serengeti imepata nafasi ya kushiriki fainali  hizo baada ya Tanzania kushinda rufaa yake dhidi ya nchi ya Congo Brazzaville ambayo ilimtumia mchezaji aliyezidi umri, Langa Lesse Bercy, katika mchezo dhidi yao wa kufuzu kucheza fainali hizo.

Watanzania tuna kila sababu ya kuhakikisha timu ya Serengeti Boys inapata maandalizi ili kufanya vizuri na hatimaye kutwaa ubingwa wa Afrika katika mashindano hayo makubwa ya Afrika.

Tayari Shirikisho la Soka Tanzania TFF, limeshatangaza kiasi cha fedha kinachohitajika  kuwa ni Sh bilioni moja kwa ajili ya maandalizi ya fainali hizo, ambapo ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki fainali hizo tangu kupata uhuru.

Tanzania tuna haja ya kujivunia kupata nafasi ya kushiriki fainali hizo lakini vile vile inatupasa kuhakikisha timu hiyo inapata maandalizi mazuri, ili iweze kushiriki nichuano hiyo bila wasiwasi na kuweza kurudi nyumbani na kikombe hicho kwa kuwa naamini kwa uwezo waliouonyesha kwenye mechi za kufuzu hilo linawezekana.

Sisi BINGWA tunaamini kwamba endapo Watanzania wote tutashirikiana katika maandalizi ya timu yetu, tuna kila sababu ya Tanzania kurudi na kombe la ubingwa wa Afrika na kuliletea sifa taifa letu, hivyo basi imefika wakati kwa watu wote kushirikiana pamoja kufanikisha mchakato huu.

Tunafahamu soka la Tanzania linakabiliwa na mizengwe, hasa katika kipindi hiki cha  kukaribia uchaguzi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), lakini  uchaguzi huo usifanye tushindwe  kuisapoti  timu yetu ya Taifa ya Vijana, Serengeti Boys.

BINGWA tunaamini kwamba kuisapoti si kwa fedha tu, michezo ipo mingi ambayo inaweza  kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika fainali hizo za Afrika, shime Watanzania, tushirikiane katika jukumu hili.

Mungu ibariki Tanzania, Serengeti Boys

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*