SANCHEZ KUTUA CITY AU MAN UNITED?

NA FAUDHIA RAMADHANI

KUMEKUWA na tetesi za nyota wa Arsenal, Alexis Sanchez, kutaka  kuondoka kwenye kikosi hicho cha Arsene Wenger, baada ya kuwasaidia kutwaa mataji ya FA na Ngao ya Jamii.

Kama mchezaji huyo mahiri wa Chile ataondoka kwenye klabu hiyo itakuwa ni pigo kubwa, hasa kutokana na kikosi cha Gunners kwa sasa kuwa kwenye mwenendo mbaya na rundo la majeruhi, huku wakiwa wamevuliwa Kombe la FA.

Kutua kwa Sanchez kwenye klabu hiyo ya Emirates mwaka 2014 akitokea Barcelona, kuliwapa mashabiki wa timu hiyo matumaini makubwa ya kuwa wanaweza kunyakua taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu wafanye hivyo msimu wa 2003/2004.

Lakini sasa nyota huyo ana kila dalili ya kuondoka na kuwaacha mashabiki hao na kiu yao ile ile ya taji.

Winga huyo alianza kuwindwa vikali na Man City inayonolewa na Pep Guardiola, ambayo inataka kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho ambacho kina nafasi kubwa ya kubeba taji la Ligi Kuu msimu huu.

Pamoja na Man City kuonekana kutaka kwa udi na uvumba saini ya mchezaji huyo wa Gunners, lakini mahasimu wao wa Jiji la Manchester, Man United wameonekana kuingilia kati na wanaweza kuvuruga kabisa mpango wa Guardiola.

Tayari Guardiola alishatenga pauni milioni 35 kwa ajili ya kunasa saini ya mchezaji huyo, Sanchez, lakini kumekuwa na taarifa kwamba Man United wako tayari kutoa pauni milioni 30 pamoja na mchezaji wao Henrikh Mkhitaryan.

Pamoja na ofa hiyo kutoka kwa kikosi hicho cha Man United kinachonolewa na Jose Mourinho, mshahara wa mchezaji huyo utakuwa ni  pauni milioni 13 kwa mwaka (shilingi bilioni 39.2).

Taarifa nyingine zilizoenea kwenye mitandao kwa siku ya jana zilidai kuwa Man United wameamua kuongeza dau la kumsajili Sanchez na kufikia pauni milioni 60 na huenda wakamfanya mchezaji anayelipwa zaidi England kwa kumpa mshahara wa pauni 400, 000 kwa wiki.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*