SANAA IENDELEE KUTUMIKA KUHIFADHI, KULINDA MAZINGIRA

NA CHRISTOPHER MSEKENA


TUKIWA tunaadhimisha Siku ya Mazingira duniani, tunapaswa kuendelea kutafakari zaidi njia na mbinu za kuhifadhi na kudhibiti uharibifu, ambao umekuwa ukileta athari mbalimbali katika jamii zinazogusa maisha yetu moja kwa moja.

Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa changamoto nyingine kubwa ambayo inatulazimu kuwa na mijadala kuhusu mazingira huku watu mbalimbali maarufu wakiweka nguvu zao katika kuielimisha jamii juu ya mazingira bora kwa uhai wa vizazi vijavyo.

Sanaa kama moja ya sekta ambayo inatoa watu maarufu wengi, mchango wake ni muhimu katika hili la mazingira na ni lazima wasanii watumike ipasavyo ili kuchochea mijadala yenye tija katika suala zima la mazingira.

Naamini sanaa ina nafasi ya kugusa maisha ya watu, asilimia kubwa katika jamii yetu ni wapenzi wa sanaa kwa namna moja ama nyingine hivyo sekta hii ni mdau muhimu wa mazingira.

Kama nitakuwa sahihi muziki, soka, filamu ndiyo nyanja zenye mashabiki wengi duniani. Hakuna mtu ambaye hasikilizi muziki kama si muziki basi atakuwa ni mpenzi wa soka na kama si hivyo basi ni shabiki wa filamu na wasanii wake.

Swali ni je, tunawatumia vipi wasanii wetu wa muziki, filamu na wacheza soka nyota tulionao katika kuhakikisha ajenda ya mazingira inakwenda poa, inaifikia jamii na kuchagiza mabadiliko chanya katika kulinda mazingira?

Kama kampuni binafsi zinawatumia wasanii kunadi bidhaa zao, mastaa wa muziki na filamu wanakuwa mabalozi wa kutangaza bidhaa za kampuni fulani, kwanini nguvu iliyopo kwenye sekta ya sanaa isiingie moja kwa moja katika mazingira.

Haipendezi wasanii waishie kuandaa nyimbo za mapenzi na starehe wakati mazingira yao yanahitaji msaada wa kusemewa ili jamii ipate elimu na kuacha kuharibu mazingira. Muziki, filamu na soka ni vitu vinavyokwenda pamoja na havitakiwi kupewa wepesi katika masuala ya mazingira.

Leo Juni 5, dunia inapoadhimisha Siku ya Mazingira, tunapaswa kuendelea kutafakari zaidi na zaidi namna ambavyo sanaa yetu inaweza kuingia kwenye sekta ya mazingira na ikatumika kubadilisha mitazamo hasi juu ya mazingira.

Tunahitaji kuendelea kuona wasanii wanapata dili za utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, hakuna kinachoshindikana hasa bajeti ikawekwa mezani kisha wasanii wakaingia kazini, kufanya sanaa zenye maudhui ya kuleta mabadiliko kwenye sekta ya mazingira.

Binafsi nimevutiwa zaidi na wiki ya mazingira ilivyoanza kwa wasanii kama Chege, Shilole, Mrisho, Mpoto, Msaga Sumu, Sholo Mwamba, Mwijaku, Ruby, Mwana FA, Nikki wa Pili, Snura, Beka Flavour, Roma na wengineo kutumika katika mijadala mbalimbali ya utunzaji mazingira.

Mfano mwishoni mwa wiki iliyopita, nyota kadhaa wa Bongo Fleva na filamu walikuwa miongoni mwa wahamasishaji mazingira katika tamasha la mazingira lenye kaulimbiu Nitunze Nikutunze, lililofanyika juzi katika viwanja vya Mbagala Zahkem, Dar es Salaam.

Ni tamasha lililoonyesha namna ambavyo sanaa inaweza kutumika kama chanzo cha watu kuelewa umuhimu wa kutunza mazingira kwa kutokukata miti ovyo, hivyo kuchangia utokeaji wa majanga mbalimbali kama ukame, mafuriko nk.

Nadhani huu ni mwanzo mzuri, wasanii waendelee kupewa nafasi za kuielimisha jamii kuhusu mazingira kwa sababu naamini wana nguvu ya ushawishi na wanasikilizwa na wengi hivyo mrejesho wa kazi yao juu ya mazingira ni mkubwa.

Kwa hiyo mbali na kuwatumia viongozi wa dini na wataalamu wa mazingira, sanaa ina nafasi kubwa ya kuhakikisha mazingira yanakuwa salama sasa na kwa vizazi vijavyo.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*