Samatta azidi kuwa lulu England

MWANDISHI WETU

TIMU ipi kati ya saba itafanikiwa kunasa saini ya nahodha wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta?

Mshambuliaji huyo anayekipiga na mabingwa wa Ubelgiji, Genk, hakurudi na kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019) inayoendelea nchini Misri na badala yake, taarifa zinasema aliruhusiwa kwenda England.

Huko England inapodaiwa Samatta alikwenda mara moja, klabu tano za Ligi Kuu na tatu za Ligi Daraja la Kwanza, zimekuwa zikipigana vikumbo kuwania saini yake.

Samatta ambaye anaonyesha nia ya kwenda kucheza soka Ligi Kuu England msimu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, anamezewa mate na Aston Villa iliyopanda daraja, Leicester City na Brighton.

Msimu mzuri aliokuwa nao 2018/19, akifunga mabao 32 katika michuano yote, ikiwamo kuisaidia Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Ubelgiji, maarufu Jupiler League na kushinda Kiatu cha Dhahabu, kumechangia Samatta kuwa lulu England.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun nchini Uingereza, Aston Villa, Leicester, Brighton, Watford na Burnley, zimeonyesha nia kupata saini ya nahodha huyo wa Taifa Stars ambaye thamani yake ni Pauni milioni 12 (takribani Shilingi bilioni 35).

Timu nyingine ambazo pia zipo mbioni kunasa saini ya Samatta kwa mujibu wa gazeti lingine la Northern Echo, ni Cardiff na Middlesbrough ambazo zote zitacheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Lakini endapo Samatta ataamua kuondoka Ubelgiji na kutua England, inaaminika atacheza katika klabu inayoshiriki Ligi Kuu England, hivyo itakuwa pigo kwa Jonathan Woodgate ambaye ni kocha wa Middlesbrough na Neil Warnock, kocha wa Cardiff.

Aston Villa inatajwa kama sehemu sahihi atakayotimkia Samatta kutokana na wageni hao wa Ligi Kuu England hadi sasa wameshatumia zaidi ya pauni milioni 50 (Shilingi bilioni 144) kwa usajili na straika huyo anatajwa kama mbadala wa Tammy Abraham aliyerudi Chelsea.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*