SAM WA UKWELI AZIKWA ALIPOZIKWA MAMA YAKE

JEREMIA ERNEST,  BRIGHITER MASAKI

HATIMAYE mwili wa staa wa singo ya Sina Raha Salim Mohamed ‘Sam wa Ukweli’, umezikwa katika makaburi ya Kiwangwa, Bagamoyo mkoani Pwani baada ya kufariki dunia juzi akiwa hospitali ya Sinza Palestina, Dar es Salaam.

Mazishi hayo yalifanyika sehemu aliyozikwa mama na mjomba wake mkubwa huku Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze Ridhiwan Kikwete wasanii wa Bongo Fleva na mashabiki wakijitokeza kumzika mkali huyo.

Akizungumza na Papaso la Burudani mjomba wa marehemu Said Yanga, alisema anashukuru wasanii, mashabiki na vyombo vya habari vyote ambavyo zimeshiriki katika mazishi ya mpwa wake.

“Kwa niaba ya familia tunatoa shukrani za dhati kwa ushirikiano mliouonyesha na kujitokeza kutufariji na  tuonyesha katika kufanikisha kumpumzisha ndugu yetu, rafiki yetu, Salim,” alisema mjomba Yanga.

Kabla ya mwili kutolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti Mwananyamala, mvutano mkali uliibuka kati ya ndugu na meneja wa zamani wa Sam wa Ukweli (Papaa Misifa) aliyeahidi kutoa usafiri wa kuelekea Bagamoyo bila mafanikio.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya Samwel Mbwana ‘Braton’, alishukuru japo mwitikio wa wasanii ulikuwa mdogo.

“Kutotokea kwa wasanii hapa Mwananyamala haimaanishi kuwa hawajashiriki katika msiba, sisi kama chama cha muziki wa kizazi kipya tuna michango anakusanya Soggy Doggy na Fid Q kama mratibu na itawafikia wafiwa,” alisema Braton.

Kama unafuatilia muziki wa Sam wa Ukweli utakuwa unafahamu katika nyimbo zake huwa anajiita Mjukuu wa Bonere ambaye ni bibi yake aliyetoa ombi la mwili wa msanii huyo uoshewe Bagamoyo ili apate nafasi ya kumwona na kumwaga kabla kuzikwa jana majira ya saa 10 jioni.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*