SAKATA LA KESSY SASA LIFIKE TAMATI

USAJILI wa beki wa kulia wa Yanga, Hassan Ramadhani ‘Kessy’ kutoka klabu yake ya zamani ya Simba, liliibua mgogoro mkubwa ambao bado unaendelea kufukuta ndani ya TFF kwa takribani miezi mitano sasa. Licha ya kwamba usajili wake ulionekana kutokuwa na shida hali iliyofanya TFF kumuidhinisha kuitumikia Yanga, lakini mwajiri wake wa zamani Simba, aliibua malalamiko mapya ambayo yaliendeleza utata wa usajili wa beki huyo.

Tayari Kessy anaitumikia Yanga lakini mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara bado hawajamalizana na Simba ambayo iliwasilisha madai TFF juu ya ukiukwaji wa vifungu vya mkataba wa mchezaji huyo.

Klabu hizo mbili zimeshindwa kufikia mwafaka wa kulipana fedha ambazo Simba wanadai, hali ambayo imelifanya suala hilo kuonekana gumu na kuendelea kushika hatamu katika midomo ya mashabiki na wadau wa soka hapa nchini.

Licha ya kuundwa kamati za mawakili wa pande zote mbili chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), wakili Said El-Maamry lakini hakuna mwafaka uliofikiwa na sasa suala hilo limerudi mikononi mwa TFF ambapo yameibuka madai mengine tena juu ya malipo ya mishahara ya mchezaji huyo.

BINGWA tunaliona sakata hili likiendelea zaidi hasa kama TFF na kamati yake husika wataendelea kuyumbayumba badala ya kusimamia kanuni na sheria zinazowaongoza katika kufanya uamuzi wa haki. Tunaamini TFF inalifahamu vizuri sana suala hili na ina uwezo wa kulitolea uamuzi kwa kuzingatia sheria, lakini imekuwa ikiyumba kutokana na kutaka kufanya mambo nje ya kanuni na taratibu.

Tungependa kuona TFF inafanya uamuzi wa suala hili na linakwisha na ambaye hataridhika akakate rufaa kwenye vyombo vinavyohusika ili suala hilo liwe limefungwa rasmi na linaondoka mikononi mwa TFF, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kulea mambo au kukaa nayo kwa muda mrefu bila sababu za msingi.

BINGWA tunaamini kwamba sheria na kanuni ziko wazi ndiyo maana TFF ilimuidhinisha kucheza Yanga, hivyo kama kuna suala jingine basi ni vyema kanuni zikatumika pia kuliamua badala ya kutaka kutumia busara ambazo mara zote zimekuwa zikisababisha lawama kwa TFF.

Ni vyema suala hilo sasa likaamuliwa na kufikia mwisho, ili hata Kessy mwenyewe awe na amani katika kuitumikia klabu yake ya Yanga au ajue nini cha kufanya pindi uamuzi utakapokuwa tofauti na ule uliomruhusu kuichezea Yanga. Lakini pia Yanga wajue cha kufanya ili isije kutokea wakalazimika kunyang’anywa pointi katika michezo ambayo wamemtumia Kessy.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*