googleAds

SABABU TATU ZA TAIFA STARS KUITUNGUA UGANDA

 

 

NA MAREGES NYAMAKA


 

MCHAMBUZI wa masuala ya soka nchini, Ally Mayay, ametaja sababu tatu za kuifanya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuibuka na ushindi dhidi ya Uganda unaotarajia kupigwa kesho.

Taifa Stars tayari iko nchini Uganda kwa ajili ya kuwavaa wenyeji wao, The Cranes mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa Afrika (Afcon) mwakani nchini Cameroon.

Mayay ambaye ni mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, aliliambia BINGWA jana kwamba, kikosi hicho cha kocha Emmanuel Amunike, kina nafasi ya kupata matokeo bora licha ya rekodi kuibeba Uganda.

“Mechi ni ngumu, suala la nidhamu lilionyeshwa mapema kabisa na Amunike, idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni na Uganda kumkosa Micho (Milutin Sredojevic), ambaye anatujua vizuri niseme tuna nafasi ya kupata matokeo bora,” alisema.

Alisema pamoja na Uganda kuwa na wachezaji 18 wanaocheza nje ya nchi, kwa sasa wana kocha mpya Mfaransa  Sebastien Desabre, ambaye ni mchezo wake wa kwanza, akidai ni faida kwa Stars tofauti na Micho.

Anaongeza kuwa wastani mzuri alionao Mbwana Samatta kufunga mabao mfululizo kwenye kikosi chake cha Genk ya Ubelgiji pamoja na pacha wake, Thomas ulimwengu, hiyo ni silaha kubwa ya Amunike.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha timu ya mwisho kuifunga Uganda uwanja wake wa nyumbani, Nelson Mandela, zamani Namboole mwaka huu ni Namibia pekee  walioibuka na ushindi wa bao 1-0 Januari kwenye michuano ya (Chan).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*