googleAds

Saanya mbona ‘fresh’ tu

NA ZAITUNI KIBWANA

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limekanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mwamuzi wa mchezo wa Yanga na Simba, Martin Saanya na msaidizi wake, Samuel Mpenzu, wamefungiwa kwa miaka miwili huku wakiweka wazi kuwa suala hilo bado linachunguzwa.

Awali taarifa zilizagaa kuwa kamati ya saa 72 iliyoketi juzi iliwafungia Saanya na Mpenzu baada ya kujiridhisha kuwa waliboronga kwenye maamuzi ya mchezo huo.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema jana kuwa Saanya na Mpenzu bado wanachunguzwa, huku akikanusha vikali tetesi za kufungiwa kwa wawili hao.

Alisema waamuzi hao pamoja na Ferdinand Chacha, sasa wanachunguzwa kwa uchezeshaji wao kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

“Mbali na ripoti ya kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo iliyoonyeshwa ‘live’, bado kamati inaendelea na uchunguzi kuhusu uchezeshaji wa Saanya na wasaidizi wake kabla ya kutangaza uamuzi wake,” alisema.

Katika hatua nyingine, klabu ya Simba SC imetozwa faini ya shilingi milioni 5 na kutakiwa kufidia gharama za uharibifu uliofanywa na mashabiki wao pale kwenye Uwanja wa Taifa.

“Kamati imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo hivyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza mechi bila mashabiki,” alisema.

Pia kamati hiyo imefuta adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Nahodha wa Simba, Jonas Mkude, baada ya kamati hiyo kuthibitisha kuwa hakustahili kadi hiyo.

“Kwa mujibu wa Kanuni ya 9 kipengele cha nane ya ligi, Kamati imemfutia adhabu Mkude baada ya kujiridhisha kuwa hakustahili adhabu hiyo,” alisema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Simba, Haji Manara, amekumbana na adhabu ya faini ya Sh 200,000 kwa kuingia uwanjani baada ya mechi hiyo wakati hakuwa miongoni mwa maofisa wa mchezo huo waliotakiwa kuwepo katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine, Azam, imepigwa faini ya Sh 3,000,000 kwa kuvaa nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu kwenye mkono mmoja tu badala ya mikono yote miwili ambapo ni kinyume na kanuni ya 13 (1).

Timu ya JKT Ruvu nayo imekumbana na rungu hilo baada ya kupigwa faini ya Sh 500,000 sambamba na shabiki wa timu hiyo kufungiwa miezi 12 kutokana na kumshambulia msimamizi wa kituo na Ofisa wa Bodi ya Ligi katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyofanyika Uwanja wa Mabatini.

Mwamuzi, Ahmed Seif, amefungiwa miezi sita aliyechezesha mchezo wa African Lyon na Mbao FC kwa kosa la kushindwa kumudu mechi hiyo ikiwemo kutoa adhabu ya penalti ambayo haikuwa sahihi, pia mwamuzi huyo alipata alama za chini ambazo hazimruhusu kuendelea kuchezesha mechi za Ligi Kuu Bara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*