Ruvu Shooting: Tunasubiri tarehe rasmi ya Ligi Kuu Bara

NA VICTORIA GODFREY

UONGOZI wa timu ya Ruvu Shooting, umesema unasubiri tamko la Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ipange tarehe ya kuendelea kwa Ligi Kuu Bara, ndipo wajue wanavipanga vipi.

Machi 17, mwaka huu, Serikali ilipiga marufuku  shughuli za mikusanyiko, ikiwamo michezo kutokana na hofu ya kuenea kwa virus vya corona.

Hatimaye, jana Rais Dk. John Magufuli, ametangaza kuruhusu ligi mbalimbali ziendelee kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema kuwa wachezaji wapo tayari muda wote kupambana kutokana na mazoezi binafsi ambayo walikuwa wanafanya kipindi ambacho Serikali ilisimamisha michezo.

“Tuliwarejesha makwao kutokana na janga hilo na tuna imani wamefanya mazoezi yao vizuri kwa kufuata program zilizokuwa zinatolewa na mwalimu Salum Mayanga na alisema wiki mbili zinatosha kucheza kitimu na kurekebisha makosa madogo madogo,” alisema Bwire. 

Bwire alisema kuwa mpango wao ni kuwarejesha wachezaji wao mara moja ili waweze kuingia kambini kuanza mazoezi ya pamoja na mwalimu kujiandaa na ligi hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*