RONALDO NYIE, AWEKA REKODI NYINGINE UEFA

TURIN, Italia

JUZI, Cristiano Ronaldo alifunga mara mbili na kuiwezesha Real Madrid kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Juventus na staa huyo aliweka rekodi mpya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mkali huyo mwenye umri wa miaka 33, amekuwa mchezaji wa kwanza kupasia nyavu katika mechi 10 mfululizo za michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa).

Aliyekuwa akiishikilia rekodi hiyo ni fowadi wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, Ruud van Nistelrooy, ambaye alikuwa amefunga katika mechi tisa mfululizo katika msimu wa 2002-03.

Mfumania nyavu huyo alianza kufungua karamu ya mabao katika dakika ya tatu tu ya mchezo huo wa kwanza wa robo fainali uliochezwa jijini Turin, kwa kuimalizia vizuri krosi ya chini kutoka kwa Isco.

Tangu alipotupia mabao mawili katika fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Juve msimu uliopita, Ronaldo amefululiza kutupia kambani mara 16 hadi kufikia sasa.

Msimu huu Ronaldo ana mabao 14 katika michuano hiyo, akiwa ametimiza mabao 23 katika mechi 14 za mwisho za Ligi ya Mabingwa, jumla akiwa na 118 katika michuano hiyo.

Aidha, nyota huyo juzi usiku aliweka rekodi ya kufungwa mabao 58 katika hatua ya mtoano, akimzidi mpinzani wake wa muda mrefu, Lionel Messi, kwa tofauti ya mabao 20.

Bao la mapema alilowafunga Juventus lilikuwa ni la 38 kwa ujumla msimu huu, ikiwa na maana kwamba Mreno huyo amefunga mabao mengi katika michuano yote Ulaya kuliko mchezaji yeyote anayecheza katika ligi tano kubwa barani humo.

Messi alikuwa na nafasi ya kuzifukuzia rekodi hizo za Ronaldo usiku wa kuamkia leo, ambapo timu yake ya Barcelona ilikuwa dimbani kuivaa Roma kwenye mchezo mwingine wa robo fainali ya michuano hiyo.

Mchezo huo dhidi ya Juve juzi, ulikuwa ni wa 27 kati ya mechi 33 za Ligi ya Mabingwa ambao Ronaldo aliweka rekodi nyingine maridhawa ya kufunga ama kutoa asisti, tangu Madrid ilipofungwa na Juve mwaka 2015.

Katika hizo mechi 33, Ronaldo amefunga jumla ya mabao 42!

Unadhani rekodi zimemalizika? Bado zinaendelea.

Ronaldo pia aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi dhidi ya timu moja katika michuano hiyo.

Mabao yake mawili dhidi ya Juventus yalimfanya Ronaldo aungane na Messi katika rekodi hiyo.

Ronaldo alifikisha jumla ya mabao tisa dhidi ya Juventus, huku Messi naye akiwa na idadi hiyo hiyo aliyofunga dhidi ya Arsenal.

Katika hali ya kushangaza, Ronaldo aliifikia rekodi yake mwenyewe ya kufungwa mabao tisa dhidi ya timu nyingine katika michuano hiyo, Bayern Munich.

Lakini, inaonekana ni kwamba mshambuliaji huyo wa zamani wa Man United anapenda kutupia dhidi ya Juve, kwani amefanya hivyo katika mechi zote tano za mwisho alizokutana nao.

Wakati wadau wa soka wakiwa ndio wanaingia kwenye maeneo ya kutazama soka usiku wa kuamkia jana, hata bila kupumua vizuri wakakaribishwa na bao la mapema la Ronaldo.

Hiyo ilikuwa ni rekodi nyingine kwa Mreno huyo.

Ronaldo alifunga bao la mapema zaidi Ligi ya Mabingwa Ulaya katika muda wake wote wa kucheza soka.

Supastaa huyo alitumia dakika mbili na sekunde 47 kuiunganisha krosi ya chini kutoka kwa Isco, na kupachika bao la mapema huku akimuacha kipa wa Juve, Gianluigi Buffon akiufuata bila mafanikio.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*