Ronaldo amfikia Messi kwa ‘hat-trick’ UEFA

ROMA, Italia

STRAIKA Cristiano Ronaldo ameifikia rekodi ya nyota mwenzake, Lionel Messi, kwa kutupia  ‘hat trick’ ya nane katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ronaldo alifikia rekodi hiyo ya nyota wa  Barcelona usiku wa kuamkia jana, baada ya kuifungia Juventus mabao hayo matatu yaliyowatupa nje ya michuano hiyo, Atletico Madrid kwa jumla ya mabao 3-2 na hivyo kutinga hatua ya robo fainali.

Messi aliweka rekodi hiyo kama ya  Ronaldo Septemba mwaka jana wakati  Barca ilipoichapa mabao 4-0 PSV.

Kabla ya kupata ushindi huo, Juve ilipoteza mchezo wa kwanza wa hatua hiyo ya 16 bora dhidi ya timu hiyo ya Atletico uliofanyika mjini Madrid, lakini mshindi huyo wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia, Ballon d’Or, Ronaldo akaweza kufuta makosa hayo na kuwafungia mabingwa hao wa Italia mabao hayo yaliyowapa ushindi wa 3-0 wakiwa nyumbani mjini Turin.

Katika mchezo huo, Ronaldo alifunga bao lake la kwanza dakika ya 27 kabla ya kumchambua tena mlinda mlango wa Atletico, Jan Oblak dakika ya nne kipindi cha pili.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 34, alikamilisha idadi hiyo kwa mkwaju wa penalti zikiwa zimebaki dakika nne kabla ya mpira kumalizika na hivyo kufikisha pia mabao 124 aliyofunga katika michezo 160 ya michuano hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*