Robbie Keane Mwanamuziki aliyetamba kwenye soka

LONDON, England

MPACHIKAJI mabao wa zamani wa Tottenham na Liverpool, Robbie Keane, ametangaza rasmi kuachana na soka na sasa atakuwa kocha msaidizi wa timu yake ya taifa ya Ireland.

Keane, aliyekuwa akiichezea ATK ya Ligi Kuu India, alifikia uamuzi huo baada ya mkuu mpya wa benchi la ufundi, Mic McCarthy, kumtaka kuwa mmoja kati ya wasaidizi wake kwenye kikosi cha Ireland.

Nyota huyo aliyewahi kutamba na Inter Milan, ndiye anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi akiwa na uzi wa taifa lake hilo (146) na pia anatambulika kama mfungaji bora wa muda wote akiwa ameipa mabao 68.

Haya ni mambo mengine 10 usiyoyajua kuhusu baba huyo wa watoto wawili; Robert Ronan Cambridge Keane (9) na Hudson (3).

  1. Klabu iliyoibua kipaji chake ni Wolves ya England kupitia ‘academy’ yake na alipata nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17, ambapo alifunga mabao mawili dhidi ya Norwich City.
  2. Ukiacha mabao yake mengi, mashabiki wa Tottenham wataendelea kukumbuka alivyowahi kuzichapa na aliyekuwa kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Uholanzi, Edgar Davids. Hata hivyo, baadaye waliyamaliza.
  3. Keane, ambaye hadi anastaafu alikuwa ameshapachika mabao 325 katika mechi 737 alizocheza katika ngazi ya klabu, ana leseni ‘A’ ya ukocha inayotolewa na Uefa (Shirikisho la Soka la Uaya).
  4. Mwaka 2015, Keane aliweka wazi msimamo wake juu ya mapenzi ya jinsia moja (ushoga na usagaji), ambapo aliiomba Serikali ya Ireland kuifanyia marekebisho sheria itayoruhusu ndoa zao.
  5. Binamu yake aitwaye Jason Byrne, anashikilia rekodi ya kuwa mwanasoka wa pili kuwa na idadi kubwa ya mabao katika historia ya Ligi Kuu ya Ireland. Mashabiki wa England watakumbuka kuwa aliwahi kuichezea Cardiff City.
  6. Huyo ndiye mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 50 akiwa na timu ya taifa katika historia ya Ireland na Uingereza. Aliweka rekodi hiyo mwaka 2011 alipofunga mara mbili dhidi ya Macedonia, hivyo kuwapiku mastaa; Ian Rush, Wayne Rooney, Bobby Charlton.
  7. ATK iliyomsajili mwaka jana inanolewa na Teddy Sheringham, staa wa zamani wa Manchester United, ambaye alicheza naye kwa misimu kadhaa pale Tottenham. Sheringham alimpa Keane jezi namba 10 na unahodha wa kikosi hicho.
  8. Keane ana binamu yake aitwaye Morrissey ambaye ni mwanamuziki mwenye jina kubwa huko Ireland. Ni hapo ndipo pia kuna stori kwamba mwanasoka huyo alikuwa na kipaji cha kuimba lakini aliachana na sanaa hiyo na kugeukia kandanda.
  9. Mechi yake ya mwisho akiwa na uzi wa Ireland ni ile ya kirafiki iliyochezwa Agosti 31, 2016 kwenye Uwanja wa Aviva, ambayo waliibamiza Oman mabao 4–0, akifunga moja. Bao hilo lilimwezesha kufikisha 68, sawa na Gerd Muller kabla ya kustaafu kuichezea Ujerumani.
  10. Keane ndiye aliyekabidhiwa benchi la ufundi ATK baada ya mabosi wa timu hiyo kumtupia virago Sheringham na dakika 90 za mechi yake ya kwanza akiwa kocha mkuu, walishinda bao 1–0 dhidi ya NorthEast United.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*