googleAds

REKODI ZINAIBEBA AZAM KUELEKEA MECHI YA COASTAL

NA SALMA MPELI

Rekodi zinaonekana kuibeba Azam FC dhidi ya Coastal Union kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo, utakaopigwa kuanzia saa moja usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Azam wanatarajia kuwa wenyeji wa mchezo huo huku rekodi muhimu zikionyesha kuwabeba zaidi matajiri hao kwa mechi zote walizokutana kwenye michuano hiyo ya Ligi Kuu Bara.

Timu hizo zimekutana mara 10 kwenye mechi za ligi, mchezo wa leo ukiwa ni wa 11 lakini Azam imeshinda mara saba, huku Coastal ikishinda mchezo mmoja na wakitoka sare mara mbili.

Katika mechi zote, Azam imefunga jumla ya mabao 18 na Coastal ikifungwa mabao nane, mabao mengi yakifungwa na wachezaji wake wa zamani, John Bocco na Kipre Tchetche.

Hadi sasa Azam imefanikiwa kucheza mechi saba kwenye ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Agosti 22, mwaka huu, ikishinda michezo minne na sare tatu ikijikusanyia jumla ya pointi 15.

Coastal Union wapo kwenye nafasi ya saba kwa pointi 13 kutokana na kucheza michezo nane ikishinda mechi tatu, sare nne na kupoteza moja iliyocheza dhidi ya Yanga.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*