Reime Schemes awawinda Amber Lulu, Gigy Money, atetea muziki wa Afrika Marekani

WAKATI mwingine nakukaribisha, Jiachie na Staa Wako, safu inayokupa nafasi ya kuwauliza maswali na kupokea majibu kutoka kwa watu maarufu kwenye tasnia ya burudani ndani na nje ya nchi.

Leo tupo na Reime Schemes ambaye ni rapa na Dj anayeishi Los Angeles, Marekani akiwa msaada mkubwa kwa wasanii wa Bongo Fleva na muziki wa Afrika Mashariki kwa ujumla kwenye anga la Kimataifa, karibu.

SWALI: Denis Chumbula kutoka Iringa anauliza: “Historia yako kwa ufupi kuhusu familia mpaka ulivyoingia kwenye muziki kama rapa na Dj”.

Reime: Mara nyingi huwa sipendi kuelezea mambo yangu ya familia, huwa sipendi kuyaweka kwenye muziki lakini mimi ni msanii ninayetoka kwenye lebo inaitwa DRS Entertainment nikiwa kama C.E.O, lengo langu ni kutaka kuendelea kuwa msanii mkubwa Afrika ndiyo maana nilianzia huku huku Marekani, nimefanya shoo Ufaransa na sehemu nyingine ambazo wamenipokea vizuri.

SWALI: Abirah Topwiso kutoka Bagamoyo mkoani Pwani anauliza: “Unadhani kwanini ni ngumu kwa muziki wa Tanzania kupenya Marekani kama ambavyo Nigeria wanafanikiwa?”

Reime: Ugumu uliopo ni kwamba Bongo Fleva inashindwa kupenya kama ilivyokuwa Nigeria japo nao hawajafanikiwa sana ni kwamba msanii hawezi kutoka bila lebo, ili utoke lazima upitie kwenye lebo kubwa.

Ndiyo maana unaona kina Chris Brown ngoma zao zinasambazwa na watu wakubwa kama Sony na kampuni zingine. Tanzania hakuna lebo inayoweza kumsimamia msanii hata hapa Marekani msanii binafsi kutoka inakuwa ngumu.

Kampuni kama Roc Nation ya Jay Z, Universal Music, Young Money na nyingine kubwa ndiyo zinasimamia huo mchongo kwahiyo ukitaka kupenya lazima uwe chini yao. Kwa muziki wa Tanzania nimeona wasanii kama Diamond Platnumz na Ali Kiba wapo kwenye hizo lebo kwahiyo ni rahisi ngoma zao kusambazwa.

SWALI: Imelda Zakayo wa Butimba anauliza: “Baada ya kufanikiwa kwenye muziki una mpango gani wa kisaidia vipaji vipya?”

Reime: Ninao mpango mkubwa sana, nimeanzisha lebo ya DRS ambayo inasambaza ngoma za msanii Dee Pesa, wimbo wake wa Go Low upo kila sehemu, nimekuja kuchukua vipaji Afrika Mashariki na kuvipeleka duniani, watu wategemee makubwa kutoka kwetu.

SWALI: Paulina Emmanuel wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam anauliza: “Unaweza vipi kugawa muda wako wa kufanya kazi za kawaida, familia na muziki?”

Reime: Kila jambo na wakati wake, muziki ni kama kazi kwahiyo familia inajua ninapokwenda kwenye muziki basi nakwenda kazini sawa tu na Daktari anavyokwenda ofisini, asilimia 90 ya maisha yangu ni muziki na iliyobaki ni familia.

SWALI: Rashid Kongolo wa Morogoro anauliza: “Lebo yako ina mipango gani katika kukuza zaidi tasnia ya muziki Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla?”

Reime: Lengo ni kukuza muziki wa Afrika sababu nimeona kuna biashara kubwa harafu sasa hivi  Marekani wanaiangalia sana Afrikai sababu kuna ‘sound’ mpya. Muziki wa Marekani umesikika sana toka miaka ya 90 mpaka leo upo namba moja duniani sasa watu wanataka kusikia ‘sound’ mpya ya muziki.

SWALI: Rajab Abbakari kutoka Dodoma anauliza: “Mbali na kusimamia wasanii wewe binafsi una mikakati ipi kwenye muziki wako?”

Reime: Nimeachia wimbo wangu mpya unaitwa Thief Ah Whine, nimemshirikisha Nashoo ni ngoma kubwa ambayo ipo kwenye chati mbalimbali duniani hata huko Tanzania wameanza kuucheza kwenye redio kadhaa pia kuna kolabo kubwa kati yangu na Dee Pesa inaitwa Run Away, kwahiyo  Rajab kaa mkao wa kula.

Pia nitakuja Afrika kufanya ziara yangu inaitwa America To Africa mwezi Aprili mwakani, nitafanya shoo na kolabo na wasanii kama Amber Lulu na Gigy Money na nitatoa mafunzo ya namna ya ‘kuji-brand’ kwa wasanii wa Bongo.

Wiki ijayo tutakuwa  mwigizaji nyota Aunt Ezekiel tuma swali lako kwake kupitia namba hapo juu


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*