REAL MADRID KWENYE ANGUKO LA AIBU

MADRID, Hispania


Zinedine Zidane

KUFUATIA kichapo cha bao 1-0 walichokipata mabingwa watetezi wa La Liga, Real Madrid dhidi ya Villarreal kwenye mchezo uliopigwa katika dimba la Santiago Bernabeu, inaonekana wazi kuwa miamba hao wanaelekea kwenye anguko la aibu msimu huu.

Licha ya kujaribu mashuti kadhaa kipindi cha kwanza kupitia kwa Marcelo na Cristiano Ronaldo, Madrid ilishindwa kabisa kufurukuta mbele ya umati wa mashabiki wao waliofurika Bernabeu.

Kichapo hicho kilizidi kuongeza presha katika benchi la ufundi la Madrid linaloongozwa na kocha Zinedine Zidane. Takwimu zinazowahusu hadi kufikia sasa zinaonesha jinsi gani wanavyoelekea kwenye anguko.

Licha ya kwamba Madrid ina mchezo mmoja mkononi, bado kazi wanayo kuwafikia vinara wa La Liga, Barcelona, ambao jana walitarajiwa kucheza dhidi ya Real Sociedad.

Kwa matokeo yoyote ya jana baina ya Barca na Sociedad, ukweli ni kwamba pengo la pointi baina ya vinara hao na Madrid ni kubwa mno kwa mabingwa hao watetezi katika nusu ya kwanza tu ya msimu.

Rekodi ya awali ilikuwa ni ya msimu wa 2012/13 ambapo kikosi cha Jose Mourinho kiliporomoka hadi nafasi ambayo walijikuta wakiwa nyuma ya Barca kwa tofauti ya pointi 18.

Msimu huu hali inaonekana kuwa mbaya kwa mabingwa watetezi hao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo katika nusu ya kwanza ya msimu wa LaLiga tayari wameshapoteza pointi 22 muhimu kutokana na sare tano na vipigo vinne walivyokutana navyo.

Tukirudi nyuma katika msimu uliopita wa 2016/17, Los Blancos hao walichukua ubingwa na pointi walizopoteza ndani ya msimu mzima zilikuwa ni 21 tu.

Kwa takwimu hiyo, ni wazi kinachofanyika chini ya Zidane si cha kuvumiliwa na timu kubwa kama Madrid, labda kocha huyo afanye marekebisho ya haraka lakini ukweli ni kwamba hata wakishinda mechi zote zilizosalia za LaLiga hawatoweza kufikia pointi 93 ambazo walizipata msimu uliopita.

Kabla ya matokeo ya jana baina ya Barca na Sociedad, ilionekana wazi kuwa Madrid iko kwenye hatari ya kumaliza nusu ya kwanza ya msimu karibu kabisa na mstari wa kushuka daraja kuliko kilele cha msimamo.

Ni jambo la kushangaza na vigumu kukubaliana nalo hasa ukikumbuka ubora wa wachezaji waliopo ndani ya kikosi cha Real Madrid.

Suala la kuwauza Alvaro Morata na James Rodriguez linadaiwa kuwa ndilo linalochangia kuikosesha Madrid nguvu ya ziada katika nyakati hizi ngumu.

Si kosa sana kuwauza, lakini kushindwa kusajili wachezaji wazuri wa kukaimu nafasi zao ni kosa kubwa ambalo Madrid wamewahi kulifanya katika miaka ya hivi karibuni.

Hivi sasa mabao hayafungwi kabisa. Kichapo cha juzi kilikamilisha mechi ya pili mfululizo nyumbani bila kutikisa nyavu za wapinzani, mara ya mwisho ilikuwa ni katika msimu wa 2006/07.

Aidha, mara ya mwisho kwa miamba hao wa Hispania kufungwa mechi mbili mfululizo ndani ya dimba la Bernabeu, ilikuwa ni msimu wa 2008/09 dhidi ya Barcelona na Real Mallorca.

Madrid ni klabu ambayo kwa miaka ya hivi karibuni ilitegemewa kuwa na mwendelezo mzuri wa kuchukua mataji na Zidane alionekana kuwa ndiye mtu sahihi wa kufanya hivyo.

Matumaini hayo ni kama yale ambayo mashabiki wa Madrid waliyapata kwa makocha wengine wa nyuma, kama vile Rafael Benitez, ambaye hata hivyo alitimuliwa msimu wa 2015/16 licha ya kwamba alimaliza nusu ya kwanza ya msimu na pointi 37, tano zaidi Zidane kwa mwaka huu.

Hizi sio kwamba ni kelele za kusema Zidane anatakiwa kuondoka, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa suala la kufukuzwa huwakuta hata wale ambao huwa na takwimu nzuri.

Kingine kinachoifanya Madrid ionekane kituko msimu huu ni kuziruhusu timu nyingine kutengeneza historia mbele yao.

Ushindi wa Villarreal ulikuwa ni wa kwanza kabisa kwa ‘Nyambizi’ hao wa Manjano ndani ya dimba la Santiago Bernabeu na ushindi wa Real Betis wa bao 1-0 uliondoa ukame wa miaka 19 kwa klabu hiyo kushindwa kuifunga Madrid.

Girona imeifunga Real Madrid kwa mara ya kwanza msimu huu, timu za Fuenlabrada na Numancia zilipata sare Bernabeu, ni matokeo ambayo watayakumbuka miaka na miaka lakini kwa Madrid ni aibu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*