Raiola upande shekhe, upande ninja

NA AYOUB HINJO

HAKUNA mwizi mvivu. Unadhani aliyesema huo msemo amekosea? Hapana hakukosea ila alituachia muda wa kutafakari zaidi na zaidi.

Hakika hakuna kipindi ambacho mawakala wanafurahi kama kipindi hiki. Wakati huu ambao ligi mbalimbali zimemalizika, huku michuano kama Copa America ikimalizika na Mataifa ya Afrika yakiendelea kufanyika, wanataka nini zaidi ya kufanya udalali unaochochewa na maneno matamu mithili ya asali.

Wakati huu ndiyo ule wa maneno ya uchochezi kati ya timu na mchezaji huku wakala akiwa mchonganishi katika hilo.

Unamkumbuka wakala wa Yaya Toure alipojaribu kuelezea kuhusu mteja wake huyo kukosa raha katika timu huku akishinikiza hapewi heshima inayostahili na Manchester City, kwa hiyo anataka kuondoka.

Hakuna njia nyingine ya kupiga pesa zaidi, ukizingatia Yaya Toure kwa kipindi kile ndiyo alikuwa silaha na tegemeo pale Etihad. Wakala alifanikiwa kupiga pesa baada ya kiungo huyo kusaini mkataba mpya uliokuwa na ongezeko la mshahara mara dufu.

Sinema ambayo aliitengeneza wakala wa Paul Pogba ilikuwa tamu mno, Mwana FA katika wimbo wake wa ‘unajua unanisikia’ alisema kuwa upande shekhe, upande ninja.

Hakuwa mwingine zaidi ya Mino Raiola kuishi katika pande zote mbili hizo kama sarafu, alikuwa adui na nyota wa mchezo kwa wakati mmoja.

Juventus walimwitaji Pogba lakini hawakuwa na uwezo wa kumpa mkataba mnono zaidi, mpaka pale Manchester United walipofika na pauni milioni 89 kumchukua, Raiola aliishi katika pepo yake kwa kuvuna kiasi kikubwa cha fedha.

Karibuni tu, Raiola amefanya mahojiano na kituo kimoja cha habari huko nchini Italia, unajua alisema nini kuhusu Pogba? Inasikitisha kidogo kwa mashabiki wa Manchester United lakini ni furaha kwake.

Kitabu ambacho kilituonyesha kuwa Mino Raiola alifanikiwa kula pauni milion 41 kwenye zile 89 za uhamisho wa Pogba kwenda Manchester United kinakaribia kuchanika.

Muda umeshapita tangu apate hizo pesa, mate yake yanatamani pesa nyingine tamu kupitia Pogba. Mpaka wakati huu ambao Manchester United wameanza maandalizi ya msimu mpya, hatma ya kiungo huyo ipo nusu nusu.

Bila presha yoyote, Raiola alisema kuwa hajui lini Pogba atajiunga na wenzake ikiwa kila mmoja anajua kuwa nyota huyo wa Ufaransa anataka kuondoka Manchester United.

Kwake huu ndio muda sahihi anaouona kujipatia pesa nyingi kupitia Pogba, hana wakati mwingine tena zaidi ya kuhakikisha kipindi hiki mifuko yake inajaa bila kujali yupi anafaidika na nani anaumia.

Anatumia nafasi hii, ni mtu makini sana kwenye matukio haya, atatengeneza kila aina ya mazingira ili afanikiwe kwenye kila anachokiwaza ili akaunti yake ya benki itoe tabasamu.

Wiki za hivi karibuni kulikuwa na taarifa kuwa Matthijs de Ligt yuko mbioni kukamilisha usajili wa kujiunga na Juventus, uwezekano huo upo lakini kwa Raiola ni rahisi kuharibika.

Pengine hivi sasa yupo mezani akiongea na Juventus huku akijibu meseji za PSG, Real Madrid au Manchester United ambao wanamwitaji beki huyo kwa udi na uvumba.

Pogba na De Ligt ni wachezaji wawili ambao wanaweza kumwingizia pesa nyingi sana Raiola katika dirisha hili la usajili bila kujali wataondoka au watasalia kwenye timu zao.

Ili Pogba abaki Manchester United lazima timu hiyo iweke pauni 500,000 mezani kama mshahara, kiasi kikubwa mno cha pesa ambacho mabosi wa klabu hiyo bado wamegawanyika nusu, wapo wanataka dili hilo lifanyike, wengine hawataki.

Katika wakati huu ambao Pogba na De Ligt wanaweza kusema wanafuraha ndani ya timu zao, kwa Raiola mambo huwa tofauti kabisa, wala usishangae.

Hakuna ugumu wowote kwa Raiola ambaye alipoteza imani kwa Sir Alex Ferguson wakati akimtorosha Pogba na kumpeleka Juventus wakati ule.

Hana muda mwingine tena wa kuzionyesha sura zake mbili, kuna upande anawafurahisha na kwingine anawaliza, wala hajali, kikubwa kwake fedha tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*