PONGEZI MASHABIKI KUISAPOTI TAIFA STARS

JUZI timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, ilirejesha matumaini ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), baada ya kuifunga mabao 2-0 Cape Verde katika mchezo wa marudiano wa Kundi L, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu ya Tanzania ilipata ushindi huo baada ya kupoteza katika mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 3-0 na Cape Verde uliochezwa Ijumaa wiki iliyopita kwenye uwanja wa nchi hiyo.

Ushindi wa Taifa Stars umepokewa vizuri na Watanzania, lakini pongezi  nyingi tunazitoa kwa mashabiki ambao walijitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao, bila kujali matokeo ya mchezo wa kwanza dhidi ya Cape Verde.

BINGWA tunamtazama shabiki ni mchezaji wa 12 anayekuwa uwanjani kuhamasisha ushindi, hivyo tuna kila sababu ya kuwapongeza kwa kujitoa kuishangilia Taifa Stars.

Tunasema kwamba, uzalendo ulioonyeshwa na mashabiki kwa timu yao, hautakiwi kupita bila kuwapongeza ikizingatiwa bado Taifa Stars inahitaji nguvu zao ili kuhakikisha inashinda michezo miwili iliyosalia dhidi ya Lesotho na Uganda.

Tunaamini kwamba, mashabiki wakiendelea na hamasa  hiyo kwa timu yao, hakika  matumaini ni makubwa kwa Tanzania kufuzu fainali za mwakani.

Tukiwapongeza mashabiki kwa kuitikia wito wa kwenda kuishangilia Taifa Stars, wachezaji bado wana kazi kubwa ya kufanya vizuri katika michezo iliyobaki.

Tunasema kwamba, wachezaji wa Taifa Stars wasibweteke  na kiwango walichokionyesha katika mchezo wao dhidi ya Cape Verde kwa kuwa bado wana shughuli pevu  kuhakikisha wanapata matokeo bora dhidi ya Lesotho na baadaye Uganda.

BINGWA tunasema kwamba, wachezaji watunze viwango vyao ili hata ule mchezo wa Lesotho utakaochezwa Novemba 16, mwaka huu, wacheze kama walivyocheza na Cape Verde katika uwanja wa nyumbani juzi.

Mara nyingi tumeshuhudia mchezaji anang’ara akicheza mchezo mmoja, lakini unaofuata anacheza vibaya, hivyo hatutarajii kuona hilo, wakati Taifa Stars inakabiliwa na michezo ya kufuzu fainali za Afcon.

Tunarudia kwa kusisitiza kwamba, mashabiki  waendelee kuonyesha uzalendo kwa Taifa Stars  ili kuirahisishia ushindi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*