Pogba amwagia sifa Maguire

MANCHESTER, England

Kiungo wa Manchester United, Paul Pogba, amemwagia sifa kede kede beki mpya wa timu hiyo, Harry Maguire, baada ya kufanikiwa kikiongoza kikosi chao kuichapa Chelsea mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu England juzi.

Kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer, kilipata ushindi huo mnono dhidi ya Chelsea inayonolewa na Frank Lampard kwenye Uwanja wa Old Trafford, uliopo jijini Manchester.

Kwa kiasi kikubwa, uwapo wa Maguire uliifanya safu ya ulinzi ya United kuwa mlima mrefu kwa washambuliaji wa Chelsea, beki huyo akiwa ametua Old Trafford hivi karibuni kutoka Leicester City, kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 80 (sh bil. 220).

Na Pogba ambaye aling’ara vilivyo kipindi cha pili katika mcheoz huo wa Jumapili, aliwaambia waandishi wa habari juu ya Maguire anayekipiga katika kikosi cha timu ya Taifa ya England akisema: “Nilimwambia (Maguire) wewe ni mnyama”.

“Kusema ukweli, kama mlivyoona, amefiti katika nafasi yake na kikosi kwa ujumla kama alivyokuwa akifanya mazoezini.

“Tulizungumzia namna ya kuimiliki vizuri safu ya ulinzi na alifanya vizuri na kuelewana vilivyo na Victor (Lindelof). Ilikuwa ni mechi nzuri sana ya kuuanza msimu kwa timu nzima.” 

Marcus Rashford alifunga mabao mawili, huku mengine yakitiwa kambani na Anthony Martial na Daniel James.  


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*