PLUIJM HATAKI MCHEZO

NA MWAMVITA MTANDA


KOCHA Mkuu wa Azam FC, Hans van der Pluijm, amesema hataki mchezo wala hana muda wa kupoteza katika kikosi chake, zaidi ya kujituma kuhakikisha kinakuwa fiti zaidi, jambo ambalo litawasaidia kufanya vizuri katika msimu mpya.

Kikosi cha Azam bado kipo nchini Uganda, ambako wamekwenda kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine na tayari wameshacheza mechi kadhaa za kirafiki.

Akizungumza na BINGWA jana kwa njia ya simu, Plujim alisema anaendeleza dozi kwa kuhakikisha kuwa timu yake inakuwa sawa.

“Sina muda wa kupoteza, muda wangu nautumia kuhakikisha kila mchezaji wangu anakuwa katika hali nzuri, tupo katika mapambano, hivyo hatupaswi kulala, bali kuhakikisha tunajipanga kwa ajili ya mapambano yaliyo mbele yetu,” alisema Pluijm.

Naye Meneja wa timu hiyo, Philip Alando, alisema ziara yao inafikia tamati Jumapili, ambapo leo watavaana na kikosi cha KCC katika mechi ya kirafiki itakayochezwa Uwanja wa Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.

Aidha, Alando alisema mechi ya mwisho itakayowafungia ziara yao itakuwa dhidi ya Express, ambayo itachezwa kesho kwenye uwanja huo huo wa Makerere.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*