googleAds

Pluijm amtumia Mourinho kujitetea

NA HUSSEIN OMAR

KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm, amemtumia mwenzake wa Manchester United, Jose Mourinho, katika kutetea matokeo ya sare ya bao 1-1 ambayo timu yake iliyapata dhidi ya wapinzani wao wa jadi Simba, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania uliochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na BINGWA jana, Pluijm alisema matokeo ya sare ya Simba yaliwachanganya wachezaji wake kwa kiasi kikubwa na kusababisha wachezaji wake kununiana mara baada ya filimbi ya mwisho.

“Pamoja na yote hatutakiwi kukata tama, ni mapema sana kufanya hivyo, katika soka lolote linawezakana,” alisema Pluijm.

“Ukitazama hata mechi za Ulaya, kuna matokeo ya kushangaza, kwa mfano sare ya Manchester United dhidi ya Burnley au kichapo ilichokipata Barcelona kutoka kwa Celta Vigo.

“Ningependa mashabiki waendelee kuiunga mkono timu yao kwa nguvu zote, hatutawaangusha tena kwa sababu tutayafanyia kazi makosa na kujipanga upya,” alisisitiza Pluijm.

Alisema jukumu kubwa lililopo mbele yao ni kuongeza nguvu katika kujiandaa kikamilifu na mchezo wao ujao dhidi ya Ruvu Shooting uliopangwa kupigwa wiki ijayo.

“Kama unavyojua, mechi kati yetu na Simba ni tofauti kuanzia timu na mashabiki, tunatarajia kurejea kwa kishindo, hakuna haja ya kukata tamaa, kuna mechi nyingi zinazotukabili,” alisema Pluijm.

Alisema kwa upande wao kama benchi la ufundi, wanatakiwa kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo huo, huku akisisitiza kuwafanyia ‘surprise’ mashabiki wa timu hiyo.

Kwa sare na Simba, Yanga imejikuta ikiendelea kudorora kwenye ligi hiyo kwani hadi sasa ikiwa imecheza mechi sita, imejikusanyia pointi 11 ikiwa katika nafasi ya tano, huku Simba wakiwa kileleni na pointi zao 17, lakini ikiwa imeshuka dimbani mara saba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*