PLUIJM AIPA SHARTI YANGA

NA ZAINABU IDDY

BAADA ya Hans van der Pluijm kuiwezesha Singida United kuibania Yanga na kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha huyo amewapa sharti timu yake hiyo ya zamani ambayo inamtaka arejee Jangwani.

Pluijm ametoa sharti zito kama Yanga wanamtaka tena katika kikosi hicho alichokipa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili, baada ya kuondoka kwa kocha wao, George Lwandamina, ambaye amerejea Zesco na jana aliishuhudia timu hiyo ikishinda bao 1-0 dhidi ya Lusaka Dynamos.

Taarifa zilizopatikana jana zinasema viongozi wa Yanga wamewasiliana na Pluijm, ambaye amewataka wamlipe deni lake la Dola 50,000 (shilingi 112,613,000) ambalo linatokana na mishahara yake anayowadai mabingwa hao watetezi.

Chanzo cha habari kimeliambia BINGWA kwamba, Pluijm yuko tayari kurejea, lakini atafanya hivyo endapo atalipwa deni lake hilo analowadai.

“Yanga wamempigia babu (Pluijm) na kumtaka arejee kuziba nafasi ya Lwandamina, lakini amewaambia hataki kurejea mpaka wamlipe deni lake,” kilisema chanzo hicho cha uhakika.

Lakini pamoja na taarifa hizo uongozi wa klabu ya Singida United umeliambia BINGWA kwamba, hawako tayari kumruhusu kocha huyo kuondoka mikononi mwao.

Pamoja na Singida United kudai kuwa hawako tayari kumwachia kocha huyo, lakini kuna taarifa kwamba, Pluijm atasaini mkataba wa kujiunga na Azam FC leo, baada ya kocha wa timu hiyo ya Chamazi, Aristica Cioaba kupata timu Abu Dhabi.

Katika mchezo wa Ligi Kuu jana, Pluijm aliiongoza Singida kutoka sare ya pili na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Sare ya kwanza dhidi ya Yanga, ilikuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, ambapo ilimalizika bila ya kufungana.

Lakini kabla ya mchezo wa jana, Pluijm aliwezesha kuitoa Yanga kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (Azam Confederation Cup) kwa kuifunga kwa penalti 4-1.

Singida ndio walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya pili likifungwa na mshambuliaji Kambale Salita, akiunganisha krosi ya Kiggi Makasy.

Bao la kusawazisha la Yanga lilifungwa na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dakika ya 45, baada ya kona ya Ibrahim Ajib kupanguliwa na mlinda mlango wa Singida United, Manyika Peter na beki huyo kumalizia kwa kichwa.

Pamoja na kuwapo na taarifa za Pluijm, kocha mwingine anayehusishwa na Yanga ni Etienne Ndayiragije wa Mbao FC, ambaye jana alizua sintofahamu baada ya kutoonekana benchi la timu hiyo wakicheza dhidi ya Njombe Mji na msaidizi wake, Ahmed Ally, kuiongoza timu kushinda mabao 2-1.

Ahmed alisema hajui ni kwanini kocha wake mkuu hakuonekana ingawa walishirikiana kwenye maandalizi ya mwisho ya mechi hiyo.

Nahodha wa kikosi hicho, Yusuph Ndikumana, ambaye ni raia wa Burundi kama Ndayiragije, alisema ana matatizo ya kifamilia na mwenyekiti wa timu hiyo, Solly Njashi, alidai afya ya kocha huyo haikuwa vyema.

Tukio hilo linatokea siku chache baada ya mashabiki wa timu hiyo kutaka kocha huyo aondoke kutokana na kuwachezesha wachezaji wa Mbao B na kuwaacha wale wa kikosi cha kwanza benchi walipocheza dhidi ya Lipuli.

Lakini juzi Jumanne, uongozi wa Mbao FC ukiongozwa na mwenyekiti wao (Njashi) walifanya kikao na kuwataka mashabiki wamwombe radhi na kuweka wazi kwamba kocha huyo ataendelea kuwapo.

Lakini kutokuwapo benchi katika mechi ya jana, kumeanza kuzua hofu kuwa huenda amerejea kwao au yuko kwenye mpango wa kujiunga na Yanga, ambao wamekuwa wakimtaka kwa muda mrefu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*