Pique alia Ramos kutolimwa kadi

MADRID, Hispania

BEKI wa Barcelona, Gerard Pique, amesema kwamba anavyoona nahodha wa  Real Madrid, Sergio Ramos, alistahili kupewa kadi nyekundu katika mchezo wao wa El Clasco uliopigwa usiku wa kuamkia jana na timu hizo kutoshana nguvu  kwa kufungana bao  1-1.

Katika mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali wa michuano ya Kombe la Copa del Rey, uliopigwa katika Uwanja wa Camp Nou, Ramos, alipewa kadi ya njano dakika ya 10 na kisha akanusurika kulimwa ya pili kutokana na rafu aliyomfanyia nyota wa Barca, Arthur Melo, kabla ya baadaye kumfanyia nyingine, Luis Suarez.

Kutokana na hali hiyo, licha ya Pique kusema kwamba mwamuzi, Antonio Mateu Lahoz, alichezesha vizuri, lakini anavyodhani Ramos alipaswa kupewa kadi nyekundu.

“Kwa ujumla ameifanya mechi ikawa nzuri,” staa huyo aliwaambia waandishi wa habari.

“Lakini ilikuwa Sergio apewe kadi nyekundu, lakini sasa hatuna la kufanya,” aliongeza nyota huyo.

Barca walijikuta wakiwa nyuma wakiwa nyumbani lakini bao lililofungwa na nyota wao, Malcom, likafuta la kuongoza lililopachikwa kimiani na Lucas Vazquez.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*