PIERRE: DJUMA SI MTU MZURI

NA ALLY KAMWE, NAKURU

Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre amemtupia lawama msaidizi wake Masoud Djuma kwa kutokumwambia kama atatimuliwa kwenye klabu hiyo ya Msimbazi.

Pierre, ambaye alisusa kukaa benchi la ufundi katika mchezo wa nusu fainali ya SportPesa Super Cup dhidi ya Kakamega Home Boys, amemshutumu msaidizi wake Djuma kwa kujua taarifa za kutimuliwa kwake na kuamua kukaa kimya.

Kabla ya kocha huyo, Pierre, kuondoka mjini Nakuru, Kenya ilikokuwa ikifanyika michuano ya SportPesa Super Cup na kwenda Nairobi kupanda ndege kurejea Dar es salaam, Mfaransa huyo alifanya kikao pamoja na Djuma na kumtakia kila la kheri na majukumu ya kukinoa kikosi cha Simba, lakini akimlaumu kwa kushindwa kuwa muwazi kwa baadhi ya mambo.

Pierre amemlaumu Djuma kwa kudai kuwa alikuwa anajua mpango mzima wa yeye kutimuliwa, lakini alishindwa kumpa taarifa mapema ili ajiandae kisaikolojia.

Kigogo mmoja wa Simba ameliambia BINGWA, kuwa kabla ya Pierre kukwea pipa alikaa kikao kizito na Djuma na alionekana wazi akimlalamikia kuwa alipewa taarifa za yeye kutaka kutimuluwa, lakini akashindwa kumfikishia.

“Kocha alizungumza na Djuma kabla hajaondoka, alionekana akimlalamikia kwa kushindwa kumpa taarifa mapema za kutimuliwa kwake,” alisema kigogo huyo.

Pierre, ambaye mkataba wake na Simba umefikia tamati, ameshaondoka mjini hapa (Nakuru) kurudi jijini Dar es Salaam, huku kukiwa na taarifa kwamba ataondoka Tanzania kurudi kwao kwani hataongezewa mkataba mwingine.

Kocha huyo ameingoza Simba kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kukaa benchi kwenye mchezo mmoja wa michuano ya SportPesa dhidi ya Kariobangi Sharks, ambapo walishinda kwa matuta 3-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 0-0.

Mchezo wa nusu fainali dhidi ya Kakamega Home Boys, Mfaransa huyo alijikuta akishuhudia akiwa jukwaani na timu ikiongozwa na msaidizi wake, Djuma na Wekundu hao wa Msimbazi kutandaza soka safi na kusonga tena mbele kwa penalti 5-4.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*