PIERRE ALISHAFUKUZWA SIMBA KABLA HAJAANZA KAZI

NA EZEKIEL TENDWA

HATIMAYE Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre na msaidizi wake, Aymen Hbibi Mohammed, wameamua kufungasha mabegi yao na kuondoka kwenye kambi ya timu hiyo nchini Kenya wanakoshiriki mashindano ya Sportpesa.

 Taarifa zinadai kuwa wawili hao wamerejea jijini Dar es Salaam jana walitarajiwa kukutana  na Mohamed Dewji ‘Mo’, na kulikuwa na kila dalili kwamba wataunganisha usafiri wa kurudi makwao hiyo ikimaanisha kuwa yale yaliyokuwa yakitabiriwa yametimia.

 Kutimua makocha imekuwa ni kama fasheni hasa kwa timu kongwe za Simba na Yanga huku pia Azam FC, nao wakionekana kuiga mtindo huo ambao kwa njia moja ama nyingine haina mantiki.

 Tetesi za kocha huyo kutokuwa na maisha marefu ndani ya kikosi hicho zilikuwa zimezagaa muda mrefu kwa kile kinachodaiwa kuwa Mfaransa huyo hafundishi soka la kisasa na badala yake anahusudu soka la kujilinda.

 

Lechantre alichukua timu kutoka kwa Mcameroon, Joseph Omog, ambaye naye alikuwa akishutumiwa hivyohivyo na mbaya zaidi namna alivyokuwa akimsugulisha benchi nahodha wa zamani wa kikosi hicho Jonas Mkude.

 Mchezo wa mwisho kwa Lechantre na kocha huyo wa viungo kusimama kwenye benchi ilikuwa ni dhidi ya Kariobangi Sharks, walioshinda mabao 3-2 kwa mikwaju ya penalti lakini mchezo uliofuata dhidi ya Kakamega Home Boys, akajikuta anakuwa mtazamani jukwaani.

Mchezo huo dhidi ya Kakamega timu iliongozwa na kocha msaidizi, Mrundi Masoud Juma, huku kocha wa makipa, Muharami Mohammed, naye akimsaidia kwa ukaribu mkubwa.

Ukweli ni kwamba Lechantre ni kama alikuwa amefukuzwa kabla ya hata hajaanza kazi kwani mashabiki wa Simba walikuwa wakimtaka Djuma, apewe mikoba yote baada ya kuridhishwa na kazi nzuri aliyoifanya kwa muda mfupi.

Djuma ndiye aliyeanza kutua Simba na kulikuwa na kila dalili za yeye kupewa mikoba ya ukocha mkuu,  lakini ghafla akaletewa Mfaransa huyo na hapo mashabiki wakaanza kupiga kelele wakimtaka Mrundi huyo aachiwe jukumu hilo.

 Baadhi ya mashabiki hao wa Simba hawakuona umuhimu wowote wa Djuma kushushwa na kuwa kocha msaidizi kwani alikuwa akiifanya kazi yake vizuri na timu ilivyokuwa chini yake ilikuwa ikipata ushindi mzuri tu. 

Licha ya kwamba liliibuka suala la kwamba kocha huyo angetimuliwa kutokana na kulipwa mshahara mkubwa, lakini hata baadhi ya viongozi walionekana dhahiri kutoridhishwa na aina ya soka linalochezwa kwa sasa na timu yao.

 Kuliibuka pia taarifa kwamba  viongozi wa Simba hawapendezewi na tabia ya ukali wa kupitiliza wa kocha huyo huku pia akishutumiwa kutokupenda ushauri kutoka sehemu yoyote na badala yake anaamini mawazo yake mwenyewe.

 Kocha huyo amekuwa akishutumiwa kutotaka ushauri hata kutoka kwa msaidizi wake,  Djuma  kiasi kwamba hata kwenye mechi anaonekana kuwa karibu zaidi na kocha wa viungo huku akimtenga Mrundi huyo ambaye ndiye aliyetakiwa kumshirikisha kila kitu.

 Licha ya kwamba Lechantre, ameipa Simba ubingwa ambao waliukosa tangu msimu wa 2011/12, lakini soka linalochezwa na timu hiyo linaonekana kutokuwaridhisha mashabiki kwani limekuwa la kujilinda zaidi.

Niseme wazi bila kuficha kwamba hata mimi sikuwa nikilielewa soka la Mfaransa huyo, kwani licha ya kuwa na wachezaji wengi wenye kasi lakini mashambulizi yao wamekuwa wakiyafanya yale ya kushtukiza.

Haiwezekani timu iwe na wachezaji kama Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi, John Bocco, Shomari Kapombe, Nicholas Gyan, Haruna Niyonzima na wengine wenye kasi halafu wakacheza mpira wa kujilinda.

 Ni kweli kwamba hamu ya mashabiki wa Simba ni timu yao kutwaa ubingwa na Lechantre alilifanikisha hilo lakini wanashindwa kuvumilia kwani kila mchezo licha ya wao kuwa na kikosi bora wanakuwa na presha na kuomba mpira umalizike.

Mathalani mchezo dhidi ya Kagera Sugar, uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Simba walikabidhiwa kombe na Rais John Pombe Magufuli.

Timu ilicheza ovyo na kusababisha kushindwa kufikia malengo yao ya kumaliza ligi bila kufungwa baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar.

 Inakuwaje Simba wanacheza na Kagera Sugar, tena Uwanja wa Taifa, wanao wachezaji kama Okwi, Kichuya na Bocco, timu ishatwaa ubingwa halafu kocha unaruhusu mchezo wa kujilinda. Ni dhahiri Mfaransa naye alishajitengenezea mazingira ya kufukuzwa.

Kocha huyo hawezi kupendwa na mashabiki kwa mpira ule uliochezwa dhidi ya Kariobangi Sharks, ambao hawakufanya shambulizi lolote la maana kwani kama wapinzani wao hao wangekuwa makini shahiri dhahiri Wekundu hao wa msimbazi wangesharudi nyumbani.

Mchezo wa pili dhidi ya Kakamega Home Boys, angalau Simba walikuwa wakifika eneo la hatari la wapinzani wao. Ni kwa sababu timu ilikuwa chini ya Djuma, ambaye aliwaruhusu wachezaji wake kucheza soka la kushambulia kwa kasi na kurudi haraka kujilinda.

Hapa tukubaliane tu kwamba soka la Simba chini ya Mfaransa huyo halikuwa lile lililozoeleka likichezwa na Wanamsimbazi hao. Soka la Simba ni la pasi fupi fupi za uhakika, pamoja na kushambulia kwa kasi kitu ambacho kilionekana kupotea ghafla.

 Ngoja tumuone Djuma kwa kipindi hiki ataifanyia nini Simba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*