Pazi: AFCON mtihani kwa Manula

NA WINFRIDA MTOI

KIPA wa zamani wa Taifa Stars, Iddi Pazi ‘Father’, amesema Kombe la Afrika (AFCON) ni mtihani kwa kipa namba moja, Aishi Manula.

Akizungumza na BINGWA jana, Pazi alisema AFCON ni mashindano makubwa kuliko hata Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Manula alicheza akiwa na kikosi chake cha Simba kilichofika robo fainali.

Alisema licha ya Taifa Stars kuwa na makipa wengine lakini mhimili mkubwa ni Manula na bado hajapatikana wa kumpa changamoto.

Pazi alisema kutokana na hilo, kocha mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, hana budi kumuanzisha katika mechi zote za kirafiki watakazocheza kabla ya michuano hiyo kuanza. Stars wamepangiwa kucheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya wenyeji Misri na Zimbabwe.

“AFCON ni mtihani mkubwa kwa Manula, ukizingatia ndiye kipa pekee anayetegemewa, ili kufahamu kama atamudu michuano hiyo kiufasaha lazima aangaliwe katika mechi za kirafiki.

“Kati ya makipa wote watano walioondoka na kikosi, hata Manula akiumwa hakuna wa kuweza kusiamama golini na kuaminiwa, hii ni changamoto.

“Ushauri wangu kwa muda huu mchache kwasababu tumechelewa maandalizi kuliko wenzetu, kocha anatakiwa kuelekeza nguvu kwa Manula na wasaidizi wake wawilia ambao ni Metacha Mnata na Aron Kalambo,” alisema Pazi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*