Paul Makonda shujaa wa Taifa Stars aliyehamishia nguvu zake Serengeti Boys 

NA JONATHAN TITO

FEBRUARI mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza kamati ya maalumu kwa ajili ya kuhamasisha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), itakayofanyika Misri.

Kamati hiyo iliyoteuliwa na TFF ilikuwa na watu 14, huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akiwa mwenyekiti.

Wakati Makonda akiwa mwenyekiti wa kamati hiyo ya uhamasishaji, Mhandisi Hersi Said aliteuliwa kama katibu.

Wengine waliokuwa kwenye kati hiyo kama wajumbe ni mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba, Haji Manara na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro.

Wajumbe wengine walikuwa ni Farouk Barhoza, Salim Abdallah, Mohamed Nassor, Patrick Kahemele, Abdallah Bin Kleb, Tedy Mapunda, Philimon Ntaihaja, Farid Nahid na Faraji Asas.

Miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo ilikuwa kuhamasisha timu ya taifa kushinda katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi L dhidi ya Uganda, ili kukata tiketi hiyo ya kufuzu Afcon.

Katika kundi hilo, Uganda ndio walikuwa vinara wakiwa na pointi 13, wakati Stars walikuwa na pointi tano sawa na Lesotho, huku Cape Verde wakiburuza mkia na pointi zao nne.

Hivyo mchezo wa mwisho wa Stars dhidi Uganda uliochezwa Machi 24, mwaka huu, ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa kuwa timu zote tatu zilizochini ya Uganda zilikuwa na nafasi ya kufuzu.

Hivyo kamati hiyo ilikuwa na kazi moja, kuhamasisha wachezaji wa Stars na mashabiki ili kuweza kupata ushindi huo.

Ingawa uteuzi huo ulipingwa na wengi, lakini kila mmoja baadaye aliona matunda yake kwa kile Makonda alichofanya pamoja na kamati yake.

Kati ya mambo aliyofanya yeye na kamati yake ni kuwaahidi wachezaji wote Sh milioni 10 kama wakishinda mechi hiyo.

Lakini pamoja na ahadi hiyo ya kuwatia nguvu wachezaji, Makonda alitumia ushawishi wake kwa wasanii na kuwakusanya pamoja na kuhakikisha wanaujaza Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kwa asilimia 100, Makonda aliweza kufanikiwa katika tukio hilo kwa kuandaa mikutano na waandishi wa habari na wasanii ambao walihamasisha wafuasi wao kupitia mitandao ya kijamii.

Uhamasishaji huo ulisaidia kwa kiasi kikubwa na siku ya mechi mashabiki waliujaza uwanja hadi wengine kukosa nafasi na kubaki nje na jambo kubwa ni vijana wa Stars wakiongozwa na nahodha wao, Mbwana Samatta, waliiwezesha Stars kushinda mechi hiyo mabao 3-2 na kufuzu kwenye michuano hiyo.

Baada ya kamati hiyo iliyoongozwa na Makonda kufanikiwa, Rais wa TFF, Wallace Karia, alimuomba mkuu wa mkoa huyo na kamati yake kuhamishia nguvu zao kwa timu ya Serengeti Boys.

Timu hiyo ya taifa ya vijana ya Tanzania ya Serengeti Boys, inashiriki kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U-17) inayofanyika hapa nchini kuanzia Aprili 14 hadi 28, mwaka huu.

Serengeti Boys, ambayo jana ilitarajiwa kushuka dimbani dhidi ya Nigeria kwenye mchezo wa ufunguzi, wamepangwa Kundi A pamoja na Angola na Uganda, huku Kundi B likiwa na timu za Cameroon, Morocco, Senegal na Guinea.

Karia alimwomba Makonda na kamati yake kusaidia timu hiyo ili iweze kushinda katika michuano hiyo na kufuzu fainali za Kombe la Dunia za vijana zitakazofanyika Brazil.

“Naomba niwaambie rasmi, mimi kama rais wa shirikisho, nimemwomba mheshimiwa Makonda na niliomba idhini kwa Rais John Magufuli kwamba kamati yake ile iendelee na zoezi la kuhakikisha timu yetu ya vijana inafanya vizuri na Mwenyezi Mungu akijalia kama si kuchukua kombe, basi twende Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia la Vijana,” alisema Karia wiki iliyopita.

Tayari kamati hiyo imeanza kazi kwa ajili ya michuano hiyo ambayo itatumia viwanja viwili, ikiwamo Uwanja wa Taifa na Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Viwanja vya Polisi Oysterbay, Makonda alitangaza kuwa kama Serengeti Boys wakifanikiwa kushinda mechi mbili za michuano hiyo na kutinga fainali za Kombe la Dunia za vijana, kila mchezaji atapata zawadi ya Sh milioni 20.

“Mimi kwa niaba ya kamati na mlezi wa timu ya Serengeti Boys (Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi), tumekubaliana kwamba mechi mbili tutakazoshinda Serengeti Boys na tukafuzu kwenda Kombe la Dunia nchini Brazil, kila mchezaji ataondoka na milioni 20,” alisema Makonda katika mkutano huo.

Lakini pamoja na ahadi hiyo, ambayo inawezekana Mengi amekubali kushirikiana nao kutokana na ushawishi wake, pia aliandaa hafla iliyofanyika Mlimani City, ikiwa na lengo la kuendelea kuhamasisha.

Huenda kuna wanaoendelea kuona kwamba Makonda hakuwa na mchango wowote kwenye harakati za Stars kwenda Afcon kwasababu zao binafsi, lakini kwa kweli kama mwenyekiti, amesaidia kwa kiasi kikubwa kuunganisha makundi ya watu ambao walijitokeza kuishabikia uwanjani kama tulivyoona.

Tayari ameshaanza kutumia ushawishi wake kwa watu maarufu, wakiwamo wasanii kuungana pamoja na kuwahamasisha wengine kuwaunga mkono Serengeti Boys, ili kuweza kubeba ubingwa wa Afcon U-17 au kutinga nusu fainali na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Brazil.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushiriki, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2017 nchini Gabon na timu hiyo kutolewa hatua ya makundi.

Mwaka 2017, Serengeti Boys walipangwa Kundi B pamoja na Mali, Niger na Angola, ambapo walifanikiwa kushinda mechi moja, sare moja na kufungwa moja na kuishia hatua hiyo.

Wakati mwaka huu Serengeti Boys wako kundi hilo A, wakiwa na Nigeria, Angola na Uganda, kwa upande wa Kundi B kuna Cameroon, Morocco na Senegal.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*