googleAds

Papaa Zahera awapa 5 Msolla, Mwakalebela

NA MWAMVITA MTANDA

WAKATI kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, akiwa katika majukumu ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenye michuano ya Kombe la Afrika inayoendelea nchini Misri, ametega sikio kujua usajili unaondelea kwa klabu yake.

Zahera ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya DRC ambayo juzi ilifungwa mabao 2-0 na Uganda katika mchezo wa kwanza wa AFCON, anapata mawasiliano yote kuhusu usajili wa wachezaji unaoendelea Yanga kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga kwasasa wako katika harakati ya kufanya usajili utakaowawezesha kurejesha heshima ya klabu hiyo, baada ya misimu miwili kushindwa kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara na kukosa kuiwakilisha nchi kimataifa.

Hata hivyo baada ya Shirikisho la Soka (CAF) kuongeza idadi ya timu shiriki kwa michuano ya kimataifa na Yanga kuongana na Simba kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, Zahera amependekeza wachezaji ambao anahitaji wasajiliwe akiamini akiwapata yote, timu hiyo itakuwa tishio msimu ujao.

Akizungumza na BINGWA kutoka Misri jana, Zahera alisema amefurahi kuona wachezaji aliyowapendekeza katika ripoti yake kusajiliwa na viongozi wa Yanga kwa asilimia kubwa.

Zahera alisema uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti, Dkt Mshindo Msolla, na makamu wake, Fredrick Mwakalebela, wamefanya kazi nzuri kwa kufanikiwa kuwaleta wachezaji aliopendekeza.

Mkongomani huyo alisema mara nyingi anapenda kufanya kazi inayonekana, hivyo atahakikisha kwa kutumia majembe yake, lazima watachukua ubingwa wa Bara msimu ujao.

Alisema wachezaji wanaosajiliwa wanatokana na mapendekezo yake akiwemo mshambuliaji wa Alliance FC, Mapinduzi Balama.

Zahera alisema katika ripoti yake ya usajili alihitaji asajiliwe mbadala wa mshambuliaji wa timu hiyo, Heritier Makambo, aliyetimkia Horoya FC ya Guinea, na amefurahi kuletewa Mganda Juma Balinya.

“Straika ndio tegemeo kubwa katika timu, hata kama kutakuwa na mabeki wazuri, lakini wamaliziaji ni wabovu lazima mambo yaende vibaya,” alisema Zahera.

Katika hatua nyingine, Zahera alisema alipendekeza asajiliwe kipa mmoja mzawa kati ya Aaron Kalambo kutoka Tanzania Prisons na Metacha Mnata wa Mbao FC.

Alisema anahitaji kipa mmoja kati ya hao wawili atakayesaidia na Klaus Kidoki ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*