‘PAPA ZAHERA’ APATA VIBALI

NA HUSSEIN OMAR

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ‘Papa Zahera’, amesema mambo ni shwari kwa upande wake, baada ya kupatiwa vibali vya kufanyia kazi nchini na mabosi wake.

Zahera, amesaini mkataba wa miaka miwili ya kuwafundisha mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini alishindwa kuanza kazi kutokana na kukosa vibali vya kufanyia kazi na kuishi hapa nchini.

Akizungumza na BINGWA jana, kutoka katika Ubalozi wa Ufaransa, alisema anajiona yupo kamili sasa, kwani muda mrefu alitamani kukaa katika benchi la ufundi la timu hiyo wakati wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni lakini alishindwa.

“Nimeumia sana kuona timu yangu mpya imemaliza kwa vipigo mfululizo, nilikuwa sina jinsi kwa sababu kuna mambo yalikuwa hajakamilika, lakini sasa nipo kamili wapinzani wafunge mkanda, ’’ alisema Zahera.

Zahera aliwaondoa hofu mashabiki na wanachama wa timu hiyo na kuwataka wasiwe wanyonge kwani kuna mashine mpya nne kutoka nchi ya Kongo, Zimbabwe, Benin, na Kenya zitawasili nchini kuanzia wiki ijayo kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mabingwa hao wa zamani.

“Naomba mashabiki watulie wajipange kwenda Uwanja wa Ndege kuwapokea vijana, siwezi kukutajia majina lakini ni watu wa kazi na wanakuja kufanya kazi na mimi, ’’ alisema Zahera.

Katika hatua nyingine Papaa Zahera alisema amefurahishwa na uamuzi uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya timu hiyo kujitoa katika michuano ya Kombe la Kagame iliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28, mwaka huu.

“Ni wazo zuri sana kama kweli wameandika barua kuomba kujitoa, kwani wachezaji wamechoka sana, nasikia wamecheza misimu mitatu bila kupumzika binafsi nasapoti hatua hii, ’’ alisema Zahera.

Zahera alisema raha ya kushiriki mashindano ni pamoja na timu wachezaji wawe fiti kiakili, kiafya hivyo hawezi kuwalazimisha viongozi kushiriki michuano hiyo wakati wachezaji wakiwa wamechoka miili yao.

“Nimewapa mapumziko ya wiki mbili wasahau mpira kidogo, lengo wakirudi wawe timamu kiakili na kimwili kwa ajili ya kufanya maandalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ’’ alisema Zahera.

Mabingwa hao wa zamani wamejitoa katika michuano ya CECAFA Kagame Cup kwa madai kuwa na majukumu mengi yatakayowafanya wasishiriki vyema.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni baada ya siku chache waandaji michuano hiyo, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutangaza kuanza kwa michuano hiyo huku, Yanga ikipangwa kundi moja na Simba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*