googleAds

PANCHO LATINO ALIONYA KUSIFIWA BAADA YA KUFA

CHRISTOPHER MSEKENA na JEREMIA ERNEST

SIKU moja baada ya kufariki dunia alipokuwa akiogelea katika fukwe za Kisiwa cha Mbudya, Dar es Salaam, mtayarishaji wa muziki nchini, Pancho Latino, kupitia ujumbe aliouandika Twitter, Aprili 29, mwaka huu, uliwaonya wadau wa muziki kuacha tabia ya kusifia na kusapoti kazi za wasanii wanapokuwa hawapo duniani.

Ujumbe huo uliokuwa gumzo katika tasnia ya burudani, Pacho Latino alionyesha kuchukizwa na tabia hiyo ambayo ilimkatisha tamaa kwa kusema: “Kuna Watanzania hawawezi kukubali kipaji chako mpaka watu wa nje au ufe ndiyo wanaanza sifa na kukusifia, ni aibu.”

Hali kadhalika rapa wa kike aliyewahi kufanya kazi na prodyuza huyo enzi za uhai wake, Tamari Ally ‘Tammy The Baddest’, jana aliweka wazi mazungumzo aliyowahi kufanya na Pancho Latino kwa Whatsapp, yaliyoonyesha alikata tamaa na alitamani kujiua.

Pacho Latino ambaye alikuwa akifanya kazi katika studio za Bhitz, alimwambia rapa huyo akisema: “Najiakiki moto kwenye moyo wangu, natamani kujiua nakuhitaji, sioni maana ya kuishi, sababu ni ukurasa mpya naanza na wasanii wapya kabisa, nilijaribu kufuata ushauri wako wa kujishusha kuwacheki wasanii wa zamani ila nilichokutana nacho najuta kwanini niliwacheki.”

Aidha, mastaa mbalimbali wakiwamo wasanii wa muziki, filamu, viongozi wa vyama vya sanaa na Serikali wameungana kutoa pole zao kwa ndugu na jamaa wa Pancho Latino ambaye anatarajia kuzikwa Jumamosi hii nyumbani kwao Gairo, Morogoro huku msiba kwa sasa ukiendelea kuwapo maeneo wa See Breeze Appartments nyumbani kwa bosi wake Hermy B.

Miongoni mwa nyimbo kubwa alizowahi kutengeneza Pancho Latino ni Baadaye Sana (Mabeste), Baby Candy (Dully Sykes), Bye Bye, Show za Joh (Joh Makini), Msiache Kuongea, Nangoja Ageuke, Bado Nipo Nipo, Msiache Kuongea (AY na FA), Dar es Salaam Stand Up (Chid Benz), Amore (Baby Madaha), Closer (Vee Money), He we Go (Jux, Wakacha), Nimechokwa, Mdananda(Shetta), Kariakoo (Mataluma) na nyingine nyingi.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*