PAMBANO LA WATANI … KUZIONA SIMBA, YANGA 7,000/-

DEBORA MBWILO (TUDARCo) NA KELVIN SHANGALI (TUDARCo)


 

HOMA ya pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga, limezidi kupanda baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana kutangaza viingilio vya mchezo huo utakaopigwa Septemba 30, mwaka huu, huku cha chini kikiwa shilingi 7,000.

Simba ndio watakaokuwa wenyeji wa mchezo huo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TFF, Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Clifford Ndimbo, alisema mchezo huo namba 72 haujasogezwa mbele kama ilivyokuwa ikivumishwa, hivyo utachezwa tarehe hiyo iliyopangwa kuanzia saa 10:00 jioni na kwamba tiketi zitaanza kuuzwa kuanzia Septemba 20, mwaka huu.

“Tiketi hizi zitapatikana kwa kupitia kadi za Selcom, hivyo kwa yule ambaye hana kadi hizo, ahakikishe anakuwanayo ili kupata tiketi hizo,” alisema Ndimbo.

Alivitaja viingilio kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP A, shilingi 20,000 VIP B, huku VIP C ikiwa ni 20,000, wakati viti vya bluu na chungwa ni shilingi 7,000.

Ndimbo alisema Jeshi la Polisi limeahidi kuweka ulinzi wa hali ya juu kuwahakikishia usalama watakaofika uwanjani, kuanzia nje ya uwanja hadi ndani, hivyo wapenzi wa soka wasiwe na hofu, wajitokeze kwa wingi kwenye dimba hilo.

Kwa mara ya mwisho Simba na Yanga kukutana kwenye ligi hiyo, ilikuwa ni Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa na kwamba Wekundu wa Msimbazi walishinda bao 1-0, shukrani kwa bao la kichwa la Erasto Nyoni lililopeleka nderemo Msimbazi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*