OLJORO KUMALIZA HASIRA KWA ALLIANCE

 

NA JACKLINE LAIZER, ARUSHA

KOCHA Mkuu wa timu ya JKT Oljoro, Emmanuel Massawe, ameahidi kuondoka na ushindi dhidi ya Alliance katika mchezo wao wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) utakaochezwa keshokutwa katika Uwanja wa Ushirika, uliopo mjini Moshi.

JKT Oljoro itashuka dimbani kuivaa Alliance huku ikiwa na machungu ya kupoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya Dodoma FC na Biashara.

Akizungumza mjini hapa jana, Massawe alisema matokeo ya ushindi ni muhimu katika mchezo huo kwa kuwa yatawaweka katika nafasi nzuri ya kupanda daraja, hivyo wapinzani wasitarajie kuambulia ushindi ugenini.

“Kikosi kipo vizuri kwani hata wachezaji waliokuwa majeruhi afya zao zimeimarika na watacheza dhidi ya Alliance, hivyo nawaomba wapenzi na mashabiki wajitokeze kuishangilia timu yao,” alisema.

Alisema anaamini bado wana nafasi ya kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao licha ya kufungwa michezo miwili.

Kocha huyo pia aliwataka waamuzi  wachezeshe kwa haki kwa kufuata sheria 17 za soka bila ya kufanya upendeleo kwa timu yoyote.

Hata hivyo, Massawe aliwataka viongozi wa Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF) kujitokeza katika michezo ya FDL ili kuangalia madudu yanayofanywa na waamuzi kwa kuchezesha kwa upendeleo wa timu moja ili waweze kuwachukulia hatua kwani waamuzi wa hivyo ndio wanasababisha kuua soka letu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*